Kiongozi mkuu Iran ataka Israel iadhibiwe

Kiongozi Mkuu wa Iran , Ayatollah Ali Khamenei akiangalia majeneza ya wanajeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu waliouawa katika shambulio la anga la Israel kwenye jengo la ubalozi wa Iran katika mji mkuu wa Syria Damascus, wakati wa hafla ya mazishi mjini Tehran,

Muktasari:

 Asema Taifa la Israel lazima liadhibiwe kwa kushambulia ubalozi wa nchi hiyo nchini Syria

Tehran. Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, amesema Taifa la Israel lazima liadhibiwe kwa kushambulia ubalozi wa nchi hiyo nchini Syria.

Katika ongezeko la vita vya Israel na maadui zake, ndege zinazoelezwa ni za kivita kutoka nchini humo zilishambulia ubalozi mdogo wa Iran ndani ya mji mkuu wa Syria Aprili mosi.

Shambulio hilo limetajwa na Iran kuwa limeua washauri saba wa kijeshi, taarifa ya Shirika la Habari Reuters leo April 10, 2024 linaripoti.

"Wanaposhambulia ubalozi mdogo,ni sawa na kushambulia  ardhi yetu," amesema Khamenei katika hotuba yake kuadhimisha mwisho wa mwezi mtukufu wa waislamu wa Ramadhan.

"Utawala mbovu ulifanya makosa lazima uadhibiwe na itakuwa hivyo," ameongeza

Akijibu kauli hiyo ya Khamenei, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israeli, Israel Katz amesema Israel itajibu ikiwa Iran itaishambulia Israeli kutoka kwenye ardhi yake.

"Ikiwa Iran itashambulia kutoka eneo lake, Israel itajibu na kushambulia Iran," Katz amesema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Iran inaunga mkono makundi ambayo yameingia kwenye mzozo na Israel baada ya Taifa hilo kushambuliwa Oktoba 7 na Hamas jambo lililoifanya Israel kutangaza oparesheni maalumu mjini Gaza.

Takriban Wapalestina 33,360 wameuawa katika miezi sita ya mashambulizi ya Israel huko Gaza. Shambulio la Hamas la Oktoba 7 dhidi ya Israel liliua watu 1,200, kulingana na takwimu za Israel.

Kundi la Hezbollah la nchini Lebanon linaloungwa mkono na Iran  na limekuwa likirushiana risasi kila siku na Israel, huku makundi ya Iraq yakiwafyatulia risasi wanajeshi wa Marekani nchini Syria na Iraq na Wahouthi wa Yemen wakilenga meli katika Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden.

Rais wa Marekani jana amemkosoa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu's kwa namna alivyoishambulia Gaza akisema hilo ni kosa.

“Nadhani anachofanya ni makosa. Sikubaliani na mbinu yake," Biden amesema kupitia mtandao wa TV unaotumia lugha ya Kihispania nchini Marekani.

(Imeandaliwa na Baraka Loshilaa)