Vita ya Israel, Palestina yaingia siku ya 100, vifo vikizidi 24,000


Muktasari:

 Zaidi ya watu 24,000 wameuawa tangu kuanza kwa mapigano kati ya Israel na kundi la Kipalestina la Hamas mnamo Oktoba 7 mwaka jana huku vita hiyo ikiingia siku ya 100 leo.



.


Gaza. Ni siku 100 tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas Oktoba 7, 2023 ambapo adadi ya watu 24,000 wameuawa katika vita hivyo.

Zaidi ya watu  23,000 wameuawa Gaza na zaidi ya 59,000 wakijeruhiwa wakati Israel wakiuawa zaidi ya watu 1,000 huku takriban watu 1,000 wakijeruhiwa.


Kwa mujibu wa BBC, takriban asilimia 85 ya wakazi huko Gaza wameyakimbia makazi yao huku maofisa wa Gaza wakisema zaidi ya asilimia 50  ya nyumba za makazi huko Gaza zimeharibiwa.


Israel inasema imetumia zaidi ya mabomu na makombora 10,000, na kuanzisha mamia ya mashambulizi ya anga Gaza, tangu shambulio la Oktoba 7 la Hamas lililoanzisha vita.


Mapema mwaka huu, Israel ilisema haina mpango wa kusitisha mashambulizi Gaza ndani ya mwaka huu kwa kile ilichodai kwamba ni hatua za kuingamiza Hamas.


 Novemba 24 hadi 30 kulishuhudiwa kusitishwa kwa mapigano hatua iliyosimamiwa na mpatanishi Qatar, jambo lililoleta matumaini ya kuisha kwa vita.


Katika makubaliano maalumu kati ya Israel na Palestina, mateka 50 wa Israel waliachiwa huru kutoka Palestina huku wafungwa 150 waliokuwa magerezani nchini Israel wakiachiwa huru.


Watanzania wawili, Joshua Mollel (21) na Clemence Mtenga (22) waliuawa na kundi la Hamas katika siku ya kwanza ya mashambulizi nchini humo walipokuwa masomoni nchini Israel.


Juhudi za viongozi mbalimbali duniani za kusitishwa kwa mapigano hazijazaa matunda huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa hilo ni “doa juu ya ubinadamu, huku Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akikisisitiza kuwa hakuna mtu atakayeizuia nchi hiyo katika vita vyake vya kuliangamiza kundi la Hamas.