Israel kuendelea kuwasaka wapiganaji, viongozi Hamas

Waziri wa ulinzi wa Israel, Yoav Gallant
Muktasari:
- Siku chache baada ya kuuawa kwa naibu kiongozi wa Hamas, Israel imetangaza kuendelea na operesheni ya kuwasaka viongozi wa kundi hilo pamoja na wapiganaji wake.
Jerusalemu. Siku tatu baada ya kuuawa kwa naibu kiongozi wa Hamas, Saleh al-Arouri, Israel imetangaza kuendelea na operesheni ya kuwasaka viongozi wa kundi hilo pamoja na wapiganaji wake huku mashambulizi yake ya anga yakiendelea Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa Reuters, mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza jana Alhamisi, Januari 4, 2024 yaliua zaidi ya Wapalestina 20, wakiwemo 16 katika mji wa Khan Younis katika eneo la pwani la Kusini lililojaa watu waliokuwa wakikimbia kutoka maeneo mengine ya eneo hilo, maofisa wa afya wa Gaza wamesema.
Miongoni mwa waliofariki dunia ni watoto tisa, walisema. Mbali na hao, Wapalestina watano wameuawa katika shambulio la ndege la Israel kwenye gari katika kambi ya wakimbizi ya Al-Nusseirat, maofisa wa afya waliliambia Reuters.
Wakazi wa Gaza wamesema ndege na vifaru vya Israel pia vimeshambulia kambi nyingine mbili za wakimbizi na kuwafanya wengi kuelekea Kusini.
Watu wamemiminika katika kambi za wakimbizi za Al-Bureij, Al-Maghazi na Al-Nusseirat jana kufuatia mashambulizi, huku baadhi ya familia zikipanda mikokoteni ya punda iliyosheheni magodoro, mizigo na watoto huku mvua zikitajwa kutatiza zoezi la uhamaji.
Mkazi mmoja wa katikati mwa Ukanda wa Gaza amesema ndege na vifaru vya Israel vimezidisha mashambulizi yao kuelekea upande wa Mashariki wa kambi za Al-Maghazi na Al-Nusseirat.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant ameelezea hatua mpya ya vita vya Israel huko Gaza, mbinu inayolengwa zaidi Kaskazini na kuwasaka zaidi viongozi wa Hamas upande wa Kusini huku Israel ikitafuta kuwaachia huru mateka waliosalia wanaoshikiliwa na Hamas.
Gallant amesema katika taarifa yake operesheni katika eneo la Kaskazini itajumuisha uvamizi, mashambulizi ya anga na ardhini na operesheni za vikosi maalumu.
Upande wa Kusini, ambako watu wengi zaidi ya milioni 2.3 wa Gaza sasa wanaishi katika mahema na makazi mengine ya muda, lengo litakuwa katika kuwaangamiza viongozi wa Hamas na kuwaokoa mateka 132 wa Israel waliosalia kati ya 240 waliotekwa nyara Oktoba 7.
Baada ya vita, Hamas haitadhibiti tena Gaza, Gallant amesema, akiongeza kuwa eneo hilo litaendeshwa na Wapalestina ilimradi kusiwe na tishio kwa Israel.
Kwa lengo la kusaidia kuzuia mgogoro huo kuenea, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ametarajiwa kusafiri jana hadi Mashariki ya Kati kwa wiki moja ya diplomasia, imesema Wizara ya Mambo ya Nje.