Naibu kiongozi wa Hamas auawa

Naibu kiongozi wa Hamas, Sahel al-Arouri

Muktasari:

  • Sahel al-Arouri, ambaye alikuwa naibu kiongozi wa kundi la wanamgambo la Hamas ameuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Israel Kusini mwa Beirut, vyombo vya habari vya Lebanon vimeripoti.

Lebanon. Naibu kiongozi wa Hamas, Sahel al-Arouri ameuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Israel, Kusini mwa Beirut vyombo vya habari vya Lebanon vimeripoti.

Hata hivyo Israel imesisitiza kuwa kuuawa kwa kiongozi huyo halikuwa shambulio dhidi ya Lebanon, kwani ilionya kuhusu adhabu ya kifo kwa kiongozi huyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya BBC, Hamas imelaani kifo hicho, huku kundi linaloliunga mkono la Hezbollah likisema ni shambulio dhidi ya mamlaka ya Lebanon.

Waziri Mkuu wa Lebanon, ameishutumu Israel kwamba, shambulio hilo ni kujaribu kuivuta Lebanon kuingia kwenye vita dhidi yao.

Wengine waliouawa katika shambulio hilo ni makamanda wawili wa kijeshi wa Hamas na wanachama wengine wanne.

Arouri (57), ndiye kiongozi Mwandamizi wa Hamas kuuawa tangu Israel ilipopigana na kundi hilo, baada ya shambulio lake la Oktoba 7, 2023.

Wapiganaji wa Hamas walivamia Israeli na kushambulia jamii zilizo karibu na mpaka, na kuua zaidi ya watu 1,200 wengi wao wakiwa raia na kuchukua mateka takribani watu 240.

Israel ilifanya mashambulizi ya kijeshi kujibu mapigo, huku ikilenga kuiangamiza Hamas.

Tangu wakati huo, zaidi ya Wapalestina 22,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.

Iran inayaunga mkono makundi ya Hamas na Hezbollah imesema mauaji ya Arouri yatachochea ongezeko la upinzani dhidi ya Israel.

Awali Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alitangaza kuwaangamiza viongozi wa Hamas popote walipo.