10 wafariki dunia mapigano ya wakulima, wafugaji
Muktasari:
- Chanzo cha mapigano hayo kinatajwa kuwa ni kifo cha mtoto wa kiume aliyeuawa baada ya kwenda kulisha mifugo kwenye shamba la karanga.
Chad. Watu 10 wamefariki dunia katika mapigano baina ya wakulima na wafugaji kusini mwa nchi ya Chad huku chanzo cha mapigano hayo kikitajwa kifo cha mtoto wa kiume (12).
Kifo cha mtoto huyo kutoka jamii ya wafugaji aliyewapeleka kuwalisha wanyama katika shamba la mkulima wa karanga ndio chanzo cha mapigano hayo yaliyopelekea watu 10 kufariki.
Gavana wa Mkoa wa Madoul, Adoum Forteye amesema tukio hilo lilitokea Alhamisi ya Mei 25, ambapo wazazi wa marehemu waliamua kulipa kisasi kwa kuwaua wakulima tisa.
Taarifa zinasema kuwa wafugaji watano na anayetuhumiwa kumuua mtoto wamekamatwa.
Inaelezwa mara kwa mara wakulima wamekuwa wakiwatuhumu wafugaji kuwalisha mifugo mazao yao na kuyaharibu huku wafugaji nao wakisema wana haki ya asili ya kuilisha mifugo kwenye maeneo hayo.
Machafuko ya aina hii yamekuwa yakitokea mara nyingi maeneo yenye rutuba ya mpakani mwa nchi ya Chad, Cameroon na Jamhuri ya Afrika ya Kati.