13 wafariki mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine
Muktasari:
- Kufuatia mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine watu 13 wameuawa katika mashambulizi ya anga katika miji mbalimbali ya Ukraine.
Ukraine. Takriban watu 13 wameuawa kufuatia mashambulizi ya anga yanayofanywa na Urusi nchini Ukraine katika miji mbalimbali nchini Ukraine ukiwemo Kyiv.
Watu 11 akiwemo mtoto mmoja waliuawa katika shambulizi la kombora lililogonga jengo moja la ghorofa katikati mwa jiji la Uman, maafisa wamesema.
Na mwanamke na binti yake wa miaka mitatu waliuawa katika jiji la Dnipro, kwa mujibu wa meya wa eneo hilo.
Milipuko pia iliripotiwa katika mji wa Kremenchuk katikati mwa Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema jengo hilo la ghorofa ni miongoni mwa majengo 10 ya makazi ambayo yaliharibiwa huko Uman. Idara ya uokoaji ya serikali imesema mtoto aliyeuawa mjini alizaliwa mwaka 2013.
Zelensky amesema mashambulizi hayo yanaonyesha ni jinsi gani hatua zaidi za kimataifa zinahitajika kuchukuliwa dhidi ya Urusi.
"Uovu unaweza kuzuiwa na silaha watetezi (majeshi) wetu wanafanya hivyo. Na unaweza kuzuiwa kwa vikwazo, vikwazo vya kimataifa lazima viimarishwe," ameandika katika mtandao wa Twetter.
Mkuu wa utawala wa kijeshi wa mji wa Kyiv amesema hilo lilikuwa shambulio la kwanza la kombora la Urusi kwenye mji mkuu katika muda wa siku 51.
Makombora 21 kati ya 23 na ndege zisizo na rubani mbili zilidunguliwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Ukraine, maafisa wamesema katika mtandao wa Telegram.
Video iliyotumwa kwenye Telegram na Huduma ya Mipaka ya Jimbo la Ukraine ilionyesha jengo la ghorofa lililoharibiwa vibaya huko Uman baada ya mgomo.
Mkazi wa jengo moja lililoharibiwa la gorofa, Olga, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba madirisha yalilipuliwa nje ya nyumba yake "kisha mlipuko ukatokea".
Mkazi mwingine wa eneo hilo alisema alisikia mlipuko saa 04:30 kwa saa za ndani. "Kulikuwa na milipuko miwili mikali sana, kila kitu kilianza kuungua, magari yakaanza kuwaka moto," alisema mkazi huyo.
Mashambulizi hayo yametokea huku wanajeshi wa Ukraine wakisema wako tayari kufanya mashambulizi ya kijeshi wakiwa na vifaa vipya, vikiwemo vifaru, vilivyotolewa na washirika wa nchi za Magharibi.
Urusi imejitahidi kupiga hatua katika mashambulizi ya majira ya baridi ikiwa ni pamoja na vita vya miezi 10 vya kuudhibiti mji muhimu wa kimkakati wa Bakhmut.
Haijabainika mara moja Urusi ilikuwa inalenga nini katika mashambulio ya Ijumaa, lakini hapo awali ilishambulia miundombinu ya raia.
Hapo awali Moscow ilisema hailengi raia kimakusudi, lakini maelfu wamejeruhiwa na kuuawa kote Ukraine tangu uvamizi wa Urusi.
Imeandaliwa na Victor Tullo.