Aliyepandikizwa chipu kwenye ubongo aanza kutumia kompyuta kwa mawazo
Muktasari:
- Ukuaji wa teknolojia unazidi kushangaza wengi ambapo kwa sasa binadamu amefanikiwa kupandikizwa chipu kwenye ubongo kwa ajili ya kutumia kompyuta kuwaza tu.
Dar es Salaam. Siku chache zikiwa zimepita tangu bilionea Elon Musk kutangaza kufanikiwa kupandikiza chipu kwenye ubongo wa mwanadamu, kwa ajili ya kutumia kifaa kama kompyuta amedai kuwa chipu hiyo imeanza kufanya kazi.
Musk kupitia kampuni ya Neuralink amesema mtu huyo sasa anaweza kutumia kipanya ‘mouse’ cha kompyuta kwa kutumia mawazo ya ubongo.
"Maendeleo ni mazuri, mtu huyo amepata ahueni kamili na ana uwezo wa kudhibiti kipanya, kusogeza kipanya kwenye skrini kwa kufikiria tu," Musk, amebainisha kwenye mtandao wa X.
Aidha, amesisitiza kuwa mtu huyo amepona bila madhara yeyote, "Tunajaribu kupata vibonyezo vingi iwezekanavyo kwa kufikiria," Musk ameongeza kama ilivyoandikwa na Shirika la AFP.
Teknolojia ya Neuralink inafanya kazi kupitia chipu hiyo ya kisasa yenye ukubwa wa sarafu tano zilizopangwa ambazo huwekwa ndani ya ubongo wa binadamu kupitia upasuaji.
Lengo lake ni kuwasiliana na kompyuta moja kwa moja na ubongo teknolojia ambayo itawasaidia watu wenye matatizo ya kupooza.
Mwaka jana kampuni inayotekeleza hilo ilipokea idhini kutoka kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA), kwa ajili ya kufanya jaribio lake la kwanza, ambapo ilitangaza kutafuta watu wa kujitolea kupandikizwa.
Je teknolojia hii ikifika nchini uko tayari kupandikizwa?