Neuralink yapandikiza ‘chipu’ kwenye ubongo wa binadamu

Muktasari:
- Kampuni ya tajiri namba mbili duniani, Elon Musk iitwayo Neuralink imesema imepandikiza ‘chipu’ kwenye ubongo wa binadamu.
Teknolojia inazidi kukua siku hadi siku, sasa kampuni ya tajiri namba mbili duniani, Elon Musk iitwayo Neuralink imesema imepandikiza kifaa cha kiteknolojia kwenye ubongo wa binadamu.
Ingawa hajatoa maelezo kamili ya mgonjwa wala kifaa hicho, ila inatajwa ni hatua muhimu kwa kifaa kiitwacho ‘Telepathy’, chenye uwezo wa kumruhusu binadamu kutumia simu au kompyuta kwa njia ya kufikiria.
"Binadamu wa kwanza amepokea kipandikizi kutoka Neuralink jana (Januari 28, 2024) na anaendelea vizuri," Musk amesema katika chapisho kwenye mtandao wa X.
Kampuni hiyo ilipokea idhini kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) kwa ajili ya kufanya jaribio la kwanza mwaka jana 2023. Ilitangaza kutafuta watu wa kujitolea kupandikizwa.
Kupitia Neurotechnology iliyoanzishwa na bilionea huyo mwaka 2016, kampuni hiyo inalenga kujenga njia za mawasiliano ya moja kwa moja kati ya ubongo wa binadamu na kompyuta.
Shirika la Habari la AFP limesema matarajio ya kampuni hiyo ni kuongeza uwezo wa binadamu, kutibu matatizo ya neva kama vile ALS au Parkinson, na kufikia uhusiano wa kimaelewano kati ya binadamu na akili bandia.
Musk amesema watumiaji wa awali watakuwa wale waliopoteza matumizi ya viungo vyao, hivyo itawawezesha waliopooza kutumia simu za kisasa kwa akili zao haraka na bila kutumia vidole. Tovuti ya Mint imeandika.
Neuralink tayari imefanya majaribio ya kina kupandikiza ‘chipu’ kwa wanyama wakiwemo nyani.
(Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mitandao)