Figo ya nguruwe iliyopandikizwa kwa binadamu mgonjwa yafanya kazi

Figo ya nguruwe iliyopandikizwa kwa biadamu mgonjwa yafanya kazi

Muktasari:

  • Mafanikio ya majaribio hayo yamesifiwa na madaktari waliofanya upasuaji huo kuwa ni "uwezekano wa miujiza".

Washington, Marekani (AFP). Nguruwe ni mnyama ambaye nyama yake inaliwa na baadhi ya jamii, huku nyingine zikiiepuka kutokana na sababu za kiimani, na sasa timu ya madaktari nchini Marekani imeongeza changamoto katika suala hilo baada ya figo ya mnyama huyo iliyopandikizwa kwa binadamu kuonekana inafanya kazi.

Mafanikio ya majaribio hayo yamesifiwa na madaktari waliofanya upasuaji huo kuwa ni "uwezekano wa miujiza".

Upasuaji huo uliofanyika Septemba 25, ulihusisha mnyama huyo mtoaji figo aliyefanyiwa marekebisho, na mgonjwa ambaye ubongo wake ulishakufa na ambaye alikuwa katika mashine ya kupumulia.

Familia ya mgonjwa huyo iliruhusu kufanyika kwa upasuaji huo wa siku mbili, kwa lengo la kuendeleza sayansi.

"Ilifanya kile ilichotakiwa kufanya, ambacho ni kuondoa uchafu na kutengeneza mkojo," Robert Montgomery, mkurugenzi wa taasisi ya upandikizaji katika Chuo Kikuu cha New York (NYU) Langone, aliiambia AFP katika mahojiano.

Kiungo hicho cha nguruwe kiliweza kupunguza kiwango cha molecule creatinine, uchafu unaochujwa kutoka kwenye damu na kutolewa nje ya mwili kwa njia ya mkojo, kitu ambacho ni ishara muhimu ya afya ya figo kwa mgonjwa.

Montgomery alifanya upasuaji huo na wenzake kadhaa katika muda wa karibu saa mbili.

Waliunganisha figo hiyo ya nguruwe na mishipa ya damu juu ya miguu ya mgonjwa, ili kuwawezesha kuifuatilia na kuchukua sampuli.

Mgonjwa huyo alikuwa ametaka kuwa mtoaji wa kiungo na awali familia yake ilifadhaishwa ilipoambiwa kuwa kiungo cha mpendwa wao hakikuwa kinafaa, alisema Montgomery.

Lakini "walijisikia ahueni fulani kwamba hili (la kujaribisha figo ya nguruwe kwa mgonjwa wao) ni fursa nyingine ya kutoa msaada," alisema.

Mgonjwa aliondolewa katika mashine ya kupumulia na akafariki baada ya saa 54 zilizofuata za kupima.

Utafiti wa awali ulionyesha kuwa figo za nguruwe zinafaa kutumika kwa viumbe ambavyo si binadamu kwa hadi mwaka mmoja, lakini hii ilikuwa ni mara ya kwanza zimejaribishwa kwa binadamu.

Nguruwe aliyetolewa figo ni miongoni mwa mifugo iliyopitia mchakato wa marekebisho ya kuondoa jini ambazo huzalisha sukari ambayo ingeweza kusababisha kingamwili za binadamu kuhamaki na kukikataa kiungo hicho.