Mbinu kudhibiti mbwakoko, kichaa cha mbwa -2

Muktasari:
- Ili kufikia kiwango cha juu cha uchanjaji mbwa, inapendekezwa kutoa chanjo bure ili kila mtu achanje mbwa wake bila vikwazo.
Dar es Salaam. Ili kudhibiti kichaa cha mbwa na wanyama hao kuzurura mitaani, wadau wameainisha maeneo matano ya kushughulikiwa, yakihusisha sheria, ushirikiano wa kisekta, chanjo na elimu kwa jamii.
Wadau wanapendekeza uwepo wa usimamizi madhubuti wa sheria kuanzia ngazi ya mtaa ili kudhibiti mbwa wanaozurura kiholela mitaani. Sekta za mifugo, afya na wamiliki wa mbwa washirikiane kudhibiti kichaa cha mbwa, huku jamii ihamasishwe kushiriki kampeni za chanjo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa zaidi ya watu 60,000 hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani.
Februari 6, 2025, Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Tamisemi, Dk Rashid Mfaume, alisema takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha watu 900 hufariki dunia kila mwaka kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa pamoja kati ya Serikali na wadau kuangalia namna ya kudhibiti kichaa cha mbwa ifikapo mwaka 2030, alisema mwaka 2024, takribani watu 35,000 waling’atwa na mbwa.

Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk Maganga Sambo, anasema mbwa wanaozurura wako hatarini kukutana na kung’atwa na mbwa wenye kichaa cha mbwa, hivyo kuambukizwa ugonjwa huo.
“Baada ya kuambukizwa, mbwa hawa pia huanza kueneza kichaa cha mbwa kwa mbwa wengine, wanyama na binadamu,” anasema.
Alivyong’atwa na mbwa
“Nilikuwa natembea njiani, ghafla mbwa akatoka kwa kasi na kuning’ata mguuni. Sikujua cha kufanya, jirani alinishauri niende hospitali haraka,” anasimulia mkazi wa Katoma, wilayani Geita, John Maganga.
Anasema hakujua iwapo mbwa aliyemng’ata alikuwa na kichaa cha mbwa, lakini baadaye alipata taarifa kuwa mbwa huyo aliuawa baada ya kumng’ata tena mtoto, ikabainika alikuwa na dalili za kichaa.
Maganga anasema alichomwa sindano tano kwa nyakati tofauti, lakini gharama za chanjo ni kubwa kwa mwananchi asiye na uwezo, akieleza kuwa kila sindano ilimgharimu Sh30,000.
Athari kiuchumi
Dk Sambo anasema tafiti zilizofanywa na IHI na wadau wake zinaonyesha kichaa cha mbwa ni tishio kubwa la afya ya binadamu na wanyama nchini Tanzania, kikisababisha vifo takribani 700 kila mwaka, pia ni changamoto ya kiuchumi kwa waathirika na Serikali kutokana na gharama za matibabu.
Anasema chanjo za PEP ni ghali (takribani Sh30,000 kwa dozi) na hazipatikani kwa urahisi, hali inayowaweka wengi hatarini.
“Dozi zinazohitajika kukamilisha matibabu ni kati ya nne au tano, kutegemea na aina ya uchomwaji wa sindano. Ambapo kuchoma kwa njia ya msuli zinahitaji dozi tano, na kwa njia ya ngozi zinahitajika dozi nne,” anasema.

Dk Sambo anasema chanjo inayochomwa kwa msuli hutolewa siku ya kwanza, ya tatu, ya saba, ya 14 na ya 21; hali iliyochangia gharama ya usafiri, chakula na malazi kwa waliokuwa katika dozi.
Kutokana na asilimia kubwa ya wanaong’atwa kuwa ni watoto, gharama ya ziada ya mtoto na anayemshindikiza huongezeka. Watoto hukosa vipindi darasani wakati wa kutafuta chanjo au kujitibu, huku watu wazima wakikosa muda wa kufanya shughuli za kiuchumi.
Utafiti wa IHI wa mwaka 2019 unakadiria kuwa hadi 2030, chanjo za sasa zitaokoa maisha ya watu zaidi ya 6,000, lakini watu 3,500 wanaweza kufariki dunia ikiwa upatikanaji wa PEP hautaboreshwa.
Taasisi ya IHI inapendekeza kutoa chanjo za PEP bila malipo ili kupunguza vifo kwa nusu ifikapo 2030. Lakini kama chanjo za PEP zitatolewa bure, sambamba na kuchanja mbwa kwa asilimia 70, hakuna mtu ataweza kupoteza maisha ifikapo mwaka 2030.
Ufanye nini uking’atwa
Nelson Lugaimukamu, Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza, ambaye pia ni daktari wa mifugo, anasema: "Mtu uking’atwa na mbwa mtaani, toa taarifa kwa uongozi ulio karibu nao kama kwa wenyeviti na watendaji wa mitaa. Baada ya kuripoti, nenda hospitali ukapate huduma za kitabibu mapema kwa sababu hauwezi kujua mbwa huyo ana kichaa au la."
Daktari wa Mifugo Mkoa wa Geita, David Mitungi, anasema mtu anapoumwa na mbwa hatua ya kwanza ni kuosha jeraha kwa maji mengi safi na sabuni kwa angalau dakika 15.

Baada ya hapo, aliyeng’atwa na mbwa anapaswa kuwahishwa hospitali ili kupata chanjo ya kichaa cha mbwa.
Dk Mitungi anasema kichaa cha mbwa ni ugonjwa hatari unaoathiri mfumo wa fahamu, na mara nyingi husababisha kifo ikiwa tiba haitatolewa kwa wakati.
“Hata kama mbwa anaonekana hana dalili za kichaa, ni bora mtu aliyeng’atwa apate chanjo mapema,” anashauri.
Dalili za ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni homa kali, kutoweza kunywa maji, wasiwasi wa hali ya juu na hatimaye kupoteza fahamu.
Nini kifanyike
Akizungumzia kuhusu udhibiti wa kichaa cha mbwa, Dk Sambo, mtafiti wa IHI, anasema ni suala jumuishi linalohitaji ushirikiano kati ya wamiliki wa mbwa, sekta za mifugo na afya.
Anasema Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya Mwaka 2008, Sehemu ya III, kifungu cha 16(1), inawawajibisha wamiliki kuwatunza wanyama wao, ikiwa ni pamoja na kuwapa chanjo. Kifungu cha 57(1) cha sheria hiyo kinatoa adhabu kwa wanaokiuka sheria.
Kuhusu sekta ya mifugo, inapaswa kuhakikisha mbwa wanapata chanjo, huku sekta ya afya inahakikisha inatoa chanjo za kuzuia kichaa cha mbwa post-exposure prophylaxis (PEP) kwa walioung’atwa na mbwa wenye kichaa.
Akizungumzia utafiti wa IHI wa mwaka 2020, ulioongozwa na Dk Kennedy Lushasi kuhusu Usimamizi Jumuishi wa Matukio ya Kung’atwa (Integrated Bite Case Management - IBCM), anasema unaonyesha ushirikiano kati ya maofisa mifugo, wauguzi na watu waliong’atwa na mbwa (au wanyama wengine) wenye kichaa cha mbwa unaleta tija kubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Anatoa mfano akisema, wauguzi ni lazima wafanye tathmini kuona kama mgonjwa aling’atwa na mnyama mwenye kichaa cha mbwa au mbwa wa kawaida ambaye hakuwa na ugonjwa huo, pia ufuatiliaji wa chanjo kwa waathirika.
Kwa upande wa maofisa mifugo au wale wa wanyamapori, ni lazima wafuatilie kama mnyama aliyeng’ata alikuwa na ugonjwa au la, na kujua kama mnyama alichanjwa dhidi ya kichaa cha mbwa au hapana, na kutoa mrejesho kwa wauguzi.
Chanjo kwa mbwa
Akizungumzia kuhusu chanjo mkoani Geita, unaoongoza nchini kwa kuwa na mbwa 302,879, Daktari wa Mifugo wa mkoa huo, Mitungi, anasema wamekuwa wakifanya kampeni, kutoa elimu kwa wananchi na kuzuia mbwa wanaozurura mitaani.
Anasema Septemba 28 ya kila mwaka, Serikali huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kichaa cha Mbwa kwa kufanya kampeni ya kitaifa ya chanjo.
Maadhimisho hayo, anasema, yanalenga kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa kichaa cha mbwa, kuhamasisha chanjo na kuhimiza hatua za kutokomeza ugonjwa huo duniani.
Anasema Serikali inahimiza wamiliki wa mbwa kuhakikisha wanyama wao hawazururi hovyo. Mkakati mwingine ukiwa kuhakikisha mbwa wanaofugwa wanahasiwa na majike kutolewa kizazi ili kudhibiti uzalishaji holela.
Mtafiti Sambo anasema asilimia 99 ya vifo vya kichaa cha mbwa vinatokana na kung’atwa na mbwa wenye ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
“Hivyo, ukiweza kuudhibiti ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa kuchanja mbwa, automatically (moja kwa moja) unakuwa umeondoa vifo vya ugonjwa huu kwa binadamu, sababu umeudhibiti ugonjwa kutoka kwenye chanzo chake, yaani mzizi wa tatizo,” anasema, akieleza chanjo ni Sh1,500.
Akizungumza na Mwananchi Machi 25, 2025, Daktari wa Mifugo jijini Dar es Salaam, James Kawamala, anasema gharama za chanjo kwa mifugo inategemea ni nani anaitoa, kwani kwa dawa za msaada chanjo ni bure, na inapotakiwa kulipiwa ni kati ya Sh2,000 na Sh5,000.
Kwa mujibu wa mtafiti Sambo, tafiti zinaonyesha ukichanja asilimia 70 ya mbwa wote inaleta kinga tosha kwa mbwa kutoambukizwa au kutoambukiza wengine, hivyo kutokomeza kabisa ugonjwa huo.
“Ili kufikia kiwango cha juu cha uchanjaji, yaani asilimia 70 ya mbwa wote, ni muhimu kuchanja mbwa bure ili kila mtu aweze kuchanja mbwa wake bila vikwazo,” anasema.
Anasema ufanisi wa kampeni za chanjo za mbwa unategemea ushirikiano wa jamii katika kupanga ratiba zinazofaa, kubaini maeneo yanayofikika kwa urahisi na kuhimiza ushiriki wa wamiliki.
Mtafiti huyo anasema kampeni za chanjo za mbwa zimesaidia kutokomeza kichaa cha mbwa katika nchi mbalimbali duniani, akitoa mfano wa Mexico.
Anasema IHI inapendekeza kampeni za kila mwaka zichanje angalau asilimia 70, akieleza tathmini ya mikakati ya chanjo katika Mkoa wa Mara (2018–2024) inaonyesha ushirikishwaji wa jamii husika ni mbinu bora ya kuimarisha kampeni za chanjo, hatimaye kudhibiti ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
“Kama chanjo za PEP zitatolewa bure na pia mkazo mkubwa ukafanyika wa IBCM na utoaji wa chanjo za mbwa ili kudhibiti ugonjwa kwenye chanzo chake, ugonjwa wa kichaa cha mbwa unaweza kutokomezwa nchini Tanzania ifikapo 2030,” anasema.
Imeandikwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Gates Foundation