Apigwa akidaiwa kumjeruhi ‘mpenzi wake’ kwenye fumanizi

Muktasari:

  • Watu wenye hasira kali wamemshambulia mwanaume wa mika 27 baada ya yeye kuwashambulia watu wawili akiwemo “mpenzi wake” kwa kitu kinachodhaniwa kuwa kisu, katika tukio linalodaiwa kuwa ni la “fumanizi.”

Dar es Salaam/Nakuru. Mwanaume mwenye umri wa miaka 27 amenusurika kufa baada ya kushambuliwa na umati wa watu wanaodhaniwa kuwa na hasira kali, baada ya kudaiwa kumchoma kisu mpenzi wake.

Mtandao Taifa Leo Digital imeripoti kuwa tukio hilo lilitokea eneo la Kolen, Kaunti Ndogo ya Nakuru Magharibi, ambapo inadaiwa alipigwa na umati huo baada ya yeye kumchoma kisu msichana anayedaiwa kuwa ni mpenzi wake katika fumanizi ambapo pia alimjeruhi jamaa aliyekuwa na dada huyo.

Akithibitisha kutokea kwa kisa hicho, Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Nakuru Magharibi, Francis Wahome, amesema msichana huyo alikuwa anatembea na mpenzi wake mpya baada ya kutengana na yule wa zamani miezi kadhaa iliyopita.

“Mwananume huyo alipomwona mpenziwe yuko na mwanamume mwingine, alipandwa na hasira na hivyo kuanzisha ugomvi...alikimbilia kitu kinachosadikika kuwa ni kisu na kuwachomba wawili hao ambao pia wanauguza majeraha,” amesema na kuongeza;

“Baada ya wananchi kuona hivyo, ndipo walipoamua kuwasaidia majeruhi waliokuwa wanavuja damu, na kwa hasira walimkamata mtuhumiwa huyo na kuanza kumshambulia, mpaka pale alipookolewa na maofisa wa polisi waliokuwa wakifanya doria eneo hilo.”

Kwa mujibu wa kamanda huyo, watatu hao walikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Nakuru, ambako wanaendelea kupata matibabu.

“Mtuhumiwa ana hali mbaya baada ya kushambuliwa na umati wenye hasira. Waathiriwa wengine wako katika hali shwari. Bado hatujawatembelea hospitalini ili kujua ukubwa wa majeraha, kwa sasa habari kuwahusu ni siri mpaka hapo watakapotoka hospitalini,” Kamnda Wahome amesema.

Hata hivyo bosi huyo wa Polisi katika Kaunti hiyo, amesema jeshi lake tayari limeanza uchunguzi kuhusu tukio hilo la utata wa kimapenzi.

“Bado hatujapata habari kamili ikiwa watatu hao ni wanafunzi au kazi wanazofanya. Tunasubiri wapate nafuu ili uchunguzi ufanyike kwa kina,” ameongeza.