Asili ya uadui wa Taliban na Marekani-2

Muktasari:

  • Kati ya mwishoni mwa Septemba na mwanzoni mwa Oktoba 1996, ndipo Taliban walikamata hatamu ya taifa la Afghanistan, wakiongoza kutokea mji mkuu, Kabul. Kufikia mwaka 1998, Taliban walikamata asilimia 90 ya nchi nzima. Mwaka 2000, mamlaka ya Taliban ilikuwa kwenye kila pembe ya Afghanistan.

Luqman Maloto

Kati ya mwishoni mwa Septemba na mwanzoni mwa Oktoba 1996, ndipo Taliban walikamata hatamu ya taifa la Afghanistan, wakiongoza kutokea mji mkuu, Kabul. Kufikia mwaka 1998, Taliban walikamata asilimia 90 ya nchi nzima. Mwaka 2000, mamlaka ya Taliban ilikuwa kwenye kila pembe ya Afghanistan.

Taliban waliposhika hatamu Afghanistan, walianzisha Dola ya Ufalme wa Kiislamu Afghanistan, yaani Islamic Emirate of Afghanistan (IEA). Waliiondoa Dola ya Kiislamu Afghanistan (Islamic State of Afghanistan ‘ISA’). Hivyo, yalikuwa mapinduzi baina ya dola za Kiislamu, isipokuwa mrengo ulikuwa tofauti.

Tofauti ya IEA na ISA ni kuwa IEA iliyoanzishwa na Taliban, iliongoza kwa sheria kali za Kiislamu. Aina zote za muziki na filamu zilipigwa marufuku Afghanistan, wanawake hawakutakiwa kufanya kazi nje ya nyumbani kwao, vinginevyo waongozane na ndugu wa kiume. Wazinifu walipigwa mawe mpaka kufa, wanaume hawakuruhusiwa kunyoa ndevu na kadhalika.

Sheria hizo kali za Taliban ndizo zilizosababisha watu wengi kuona uongozi wa Taliban ni sawa na gereza. Muda ulivyokwenda ndivyo Taliban walivyoendelea kuzidisha makali ya uongozi na sheria kali za Uislamu.


Uadui wa Taliban na Marekani

Ipo dhana kuwa ugomvi wa Marekani na Taliban ni kwa sababu ya kikundi hicho kuongoza dola ya Kiislamu nchini Afghanistan. Ukweli ni kuwa Marekani ilishirikiana na wapiganaji wengi wa Kiislamu (mujahidina), kwa kufadhili harakati zao kuiondoa Dola ya Umoja wa Nchi za Kisovieti (USSR), iliyokuwa imeikalia Afghanistan.

Jicho baya la Marekani kwa Taliban lilianza mwaka 1996, Osama bin Laden alipopewa hifadhi salama na ulinzi juu nchini Afghanistan. Agosti 1996, Osama alitoa tamko (fatwa), la kutangaza vita dhidi ya Marekani kwa kukalia miji miwili mitakatifu kwa imani ya Kiislamu. Miji hiyo ni Makka na Madina, iliyopo Saudi Arabia.

Wakati huo, Marekani ilikuwa imeweka majeshi yake nchini Saudi Arabia. Iliweka kambi hapo tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990, Marekani ilipokuwa inakabiliana na Iraq, baada ya Saddam Hussein kuivamia Kuwait. Osama aliutafsiri ukaaji wa Marekani katika miji hiyo kuwa chukizo kubwa kwa Mungu.

Tamko hilo la vita dhidi ya Marekani, Osama alilitolea Afghanistan. Sasa, kitendo cha Taliban kumpa hifadhi Osama, vilevile kumpa uwanja kiongozi huyo wa mtandao wa Al-Qaeda, kutengeneza mipango na utekelezaji wa mashambulizi dhidi ya Marekani ni sababu ya Wamarekani kuiona Serikali ya Taliban kuwa adui yao.

Hata hivyo, hasira nyingi za Marekani kwa Taliban ziliibuka mwaka 1998. Balozi za Marekani Nairobi, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania, zilipolipuliwa na maofisa wa Al-Qaeda, Agosti 7, 1998. Ni kuanzia hapo Marekani waligeuza macho yao na kumtazama Osama kama adui yao namba moja. Osama alikuwa akiishi salama Afghanistan kwa ulinzi wa Serikali ya Taliban.

Sasa, chukua msemo kutoka kwenye lugha ya falsafa ya Kihindu, Jain, Buddha na Sikhi inayoitwa Sanskrit inayoeleza kuwa Rafiki wa Adui Yako ni Adui Yako (A Friend of Your Enemy is Your Enemy). Kwa vile Taliban walijipambanua kuwa marafiki wa Osama pamoja na mtandao wake wa Al-Qaeda, ambao ni maadui wa Marekani, ndivyo uadui ukawepo.

Kisha, Septemba 11, 2001 ikawadia. Maofisa wa Al-Qaeda kwa mara nyingine, wakaishambulia Marekani. Majengo ya Kituo cha Biashara Duniani (WTC), New York, yakashambuliwa. Marekani walitaka Taliban wamuondoe Osama nchini Afghanistan, lakini waligoma.

Kwa msimamo huo wa Taliban, Rais wa 43 wa Marekani, George W Bush (Bush Jr), alituma vikosi wa jeshi la Marekani kuivamia Afghanistan. Lengo kuu likawa kuuangusha utawala wa Taliban, vilevile kumkamata Osama, akiwa hai au amekufa, na muhimu zaidi ni kusambaratisha kitovu cha mtandao wa Al-Qaeda.

Kwa uvamizi huo, Taliban waliondoshwa Afghanistan. Marekani iliweza kusimika uongozi mpya na kufanikisha uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka 2004. Kuhakikisha Taliban hawarejei tena Afghanistan, Marekani walijipa jukumu la kutengeneza jeshi jipya la Afghanistan.


Uswahiba wa Taliban na Al-Qaeda

Kufahamu kwa nini Taliban walikubali kupambana na Marekani kuliko kumuondoa Osama na Al-Qaeda yake nchini Afghanistan, ni lazima kwanza kurejea nyuma kwenye mahali ambapo itikadi za makundi yao ilizaliwa. Ndipo utabaini kwamba Al-Qaeda na Taliban ni mapacha.

Kwanza, asili ya Al-Qaeda na Taliban ni vita ya kuwaondoa Sovieti nchini Afghanistan. Muasisi wa Taliban, Mohammed Omar (Mullah Omar), alipokea mafunzo ya kijeshi nchini Pakistan kwa ufadhili wa Marekani. Osama, aliingia Pakistan kusaidia makundi ya mujahidina ili kuwaondoa USSR nchini Afganistan.

Hivyo, miaka ya 1980 mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1990, Mullah Omar, Osama na Marekani, walikuwa na agenda moja ya kuwadhoofisha Sovieti. Osama alitumia fedha zake binafsi kufadhili wapiganaji wa mujahidina. Mullah alikuwa mnufaika wa fedha za Marekani pamoja na Osama.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, mawazo yalihama. Mullah Omar alianzisha Taliban, kwa hoja kuwa Afghanistan ilihitaji sera kali zinazotokana na mafundisho ya Kiislam. Mullah aliona kuendelea kuishi kwa muongozo wa Marekani, kungesababisha umagharibi utawale Afghanistan kuliko Uislam.

Osama baada ya kushiriki mapambano ya kuwaondoa Sovieti nchini Afghanistan, alirejea nyumbani kwao Saudi Arabia kama shujaa. Hata hivyo, baada ya kuingia Saudia, aligundua kuwa Marekani walikuwa wameweka majeshi yao kwenye miji ya Makka na Madina, kitu ambacho alikitafsiri kama dhambi kubwa.

Jicho la pili la Osama lilikuwa Lebanon na Palestina, kwamba Marekani ilikuwa inashiriki moja kwa moja kuua Waarabu. Ndio maana katika tamko la Osama la mwaka 1996, alitangaza vita dhidi ya Marekani, alikumbusha vifo vya watu wa Iraq, Palestina, Lebanon, vilevile laana ya kuweka kambi za kijeshi kwenye miji ya Makka na Madina.

Utaona kuwa Al-Qaeda na Taliban ni makundi yaliyoundwa kwa itikadi moja, kukabiliana na Marekani na kutetea kile ambacho wao walikiona ni haki juu ya Uislam. Hivyo, Taliban na Al-Qaeda ni mapacha. Haikuwa rahisi kwa Marekani kugombana na Al-Qaeda bila Taliban kuhusika.


Inaendelea….