AU rasmi mwanachama G20

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alimkaribisha Mwenyekiti wa AU, Azali Assoumani ambaye pia Rais wa Visiwa vya Comoro

Muktasari:

  • Umoja wa Afrika umekuwa kundi la pili la kikanda kuingizwa katika kundi la mataifa 20 yanayoongoza kiviwanda na yanayoendelea kama mwanachama kamili wa kudumu, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alitangaza jana Jumamosi mwanzoni mwa mkutano wa siku mbili wa viongozi wa G20 mjini Delhi.

India. Umoja wa Afrika (AU) umekuwa kundi la pili la kikanda kuingizwa katika Kundi la mataifa 20 yanayoongoza kiviwanda na yanayoendelea (G20), kama mwanachama kamili wa kudumu, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alitangaza jana Jumamosi mwanzoni mwa mkutano wa siku mbili wa viongozi wa kundi hilo unaofanyika mjini Delhi.

AU yenye wanachama 55 wa mataifa ya Afrika, inaungana na Umoja wa Ulaya (EU), kama shirika la pili la kikanda kuwa mwanachama wa kudumu wa G20.

"Uongozi wa India kwenye mkutano huu wa G20, umekuwa ishara ya ushirikishwaji, ndani ya nchi na nje, inayowakilisha moyo wa umoja," Modi alisema katika hotuba yake ya ufunguzi.

Modi alisema India imekuwa kiungo muhimu katika kushawishi AU kupewa uanachama wa kudumu kwenye G20.

Kwa kumbato la furaha ya baada ya tangazo hilo, Modi alimkaribisha Mwenyekiti wa AU Azali Assoumani ambaye pia rais wa Visiwa vya Comoro na kumpa nafasi kwenye meza ya mkutano ya wanachama wa kudumu wa G20.

"Kwa idhini ya kila mtu, namwomba mkuu wa Umoja wa Afrika kuchukua kiti chake kama mwanachama wa kudumu wa G20," alisema.

Kwa upande wake Rais wa baraza la Ulaya, Charles Michel aliipongeza AU kwa hatua yake hiyo kubwa akiandika kupitia ukurasa wa mtandao wake wa X zamani Twitter.

"EU imekuwa mfuasi thabiti wa mpango huu na nina furaha kuupigia debe tangu mwanzo na Macky Sall," aliongeza. Sall ni rais wa Senegal na alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika 2022.

Awali Afrika ilikuwa imewakilishwa kidogo tu ndani ya G20 kupitia kiti cha Afrika Kusini kabla ya umoja kupewa uanachama hapo jana.