Ahadi ya Rais Biden kwa Afrika yawagawa wasomi nchini

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mkutano wa Viongozi wa Afrika na Marekani (U.S Afirica Leaders Summit) wakati wakijadili masuala ya Kilimo, Usalama wa Chakula na Uzalishaji wa Chakula, uliofanyika katika ukumbi wa Convention Centre Jijini Washington DC nchini Marekani. Picha Ikulu

Muktasari:

Uhusiano kati ya Marekani na mataifa ya Afrika unadaiwa kudorora zaidi wakati Marekani ikiongozwa na Rais Donald Trump

Dar es Salaam. Wakati Rais wa Marekani, Joe Biden akieleza kuunga mkono Umoja wa Afrika (AU) kujiunga na kundi la mataifa yenye nguvu kiuchumi duniani (G20), wachambuzi wa masuala ya uchumi na diplomasia nchini wametoa maoni tofauti wakieleza hatua hiyo itaongeza uhusiano wa kibiashara na uchumi.

Biden alitangaza kuiunga mkono AU yenye wanachama 49 kujiunga na kundi la mataifa ya G20, huku akitaka kujenga uhusiano imara na mataifa ya Afrika.

Akizungumza katika hafla ya mkutano wa viongozi wa Marekani na Afrika juzi, Biden alisema “uongozi wa Kiafrika na uvumbuzi ni muhimu katika kushughulikia baadhi ya changamoto kubwa duniani.”

Mkutano huo ulifanyika jijini Washington D.C, Marekani kuanzia Desemba 13 hadi 15, huku ukiwa umehudhuriwa na viongozi 49 kutoka Afrika, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la Aljazeera, msukumo wa utawala wa Biden kuwekeza barani Afrika unakuja wakati kukiwa na ushindani kutoka mataifa ya China na Russia, ambao wameonekana kuwekeza katika bara hilo, kiwango ambacho kimeishinda Marekani katika miaka ya hivi karibuni.

Biden alitaka kujenga upya uhusiano wa Marekani nje ya nchi, baada ya miaka minne ya sera ya nje ya mtangulizi wake, Rais Donald Trump ya “Marekani Kwanza” ambayo ilishuhudia nchi hiyo ikijiondoa katika mashirika na makubaliano ya kimataifa.

Wakizungumza na Mwananchi, wachumi na wanadiplomasia wamesema AU ikijiunga na G20, italeta manufaa ya kiuchumi huku wengine wakiona hatua hiyo kama udhalilishaji kwa bara la Afrika.

Mhadhiri Chuo cha Diplomasia, Innocent Shoo, alisema endapo AU watakuwa miongoni mwa wanachama wa G20, nchi za Afrika zitapata manufaa makubwa, ikiwa ni kupata fursa ya kuwa na mikataba tofauti ya kibiashara, kimkakati na kidiplomasia.

Profesa Wetengere Kitojo kutoka Chuo cha Diplomasia, alisema jambo hilo ni la kisiasa zaidi.

“Ukiliangalia hili suala linaonekana ni la kisiasa zaidi, kwa maana Marekani anatafuta njia ya kujenga urafiki na Afrika, inabidi tujiulize endapo Afrika ikiwa miongoni mwa wanachama wa G20, je, itakuwa na nguvu kama mataifa mengine?” alihoji Profesa Kitojo.

Dk Abel Kinyondo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema haoni msaada wowote ambao Afrika itaupata ikiwa mwanachama wa G20.

G20 inaundwa na mataifa makubwa zaidi ya kiuchumi duniani, yakiwemo mataifa yaliyoendelea kiviwanda na yanayoendelea; inachangia karibu asilimia 80 ya pato la jumla la dunia, asilimia 75 ya biashara ya kimataifa.

Kundi hili linalojumuisha nchi 19 na Umoja wa Ulaya (EU) linafanya kazi kushughulikia masuala makuu yanayohusiana na uchumi wa dunia kama vile utulivu wa kifedha wa kimataifa, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na maendeleo endelevu.