Aua familia nzima kwa risasi baada ya mkewe kudai talaka

Muktasari:

  • Mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 42, Michael Haight wa nchini Marekani katika Jimbo la Utah, ameua familia yake ya kwa risasi na kisha mwenyewe kujiua baada ya mkewe kudai talaka.

Dar es Salaam. Mwanamume mwenye umri wa miaka 42 katika Jimbo la Utah nchini Marekani amewapiga risasi watu saba wa familia yake kabla ya kujiua mwenyewe, baada ya mkewe kudai talaka.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji za Uingereza (BBC), polisi katika jimbo hilo wamesema familia ya watu wanane ilipatikana wakiwa wamefariki ndani ya nyumba katika Jiji la Enoch Jumatano usiku wakati wa ukaguzi wa ustawi katika maeneo hayo.

Polisi wanasema waliouawa ni pamoja na mke wa mwanamume huyo, watoto wake watano na mama mkwe wake.
Meneja wa Jiji Rob Dotson amesema mji huo wenye watu wapatao 8,000 ulikuwa katika mshtuko.
Katika mkutano na wanahabari uliofanyika Alhamisi Januari 5, maofisa wa jiji hilo walisema mfanyabiashara wa bima mwenye umri wa miaka 42, Michael Haight aliwafyatulia risasi mkewe Tausha mwenye umri wa miaka 40, mama mkwe wake Gail Earl mwenye umri wa miaka 78 na watoto wake watano kabla hajajiua.


Watoto hao watano ambao hawakutajwa majina yao ni pamoja na wasichana watatu, wenye umri kuanzia miaka 17, 12 na 7, na wavulana wawili, umri 7 na 4.
Meneja wa Enoch City Rob Dotson amesema miili yao iligunduliwa na polisi siku ya Jumatano Januari 4, baada ya kuripotiwa mkewe kukosa miadi iliyoratibiwa na hivyo kusababisha ukaguzi wa ustawi wa nyumba ya familia hiyo.

Hata hivyo meneja huyo alisema kwamba kila mmoja wa waathiriwa alionekana kuwa na jeraha la risasi.
Maofisa pia walithibitisha kwamba mkewe alikuwa amewasilisha maoombi ya talaka Desemba 21, 2022.