Profesa Muhongo aomba Musoma Vijijini iwe wilaya kuchochea maendeleo
Baadhi ya majengo ya shule mpya ya Msingi Kasoma katika halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Profesa Muhongo ametoa ombi hilo leo, Jumamosi, Julai 4, 2026, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Suguti na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba
Musoma. Mbunge wa Musoma Vijijini mkoani Mara, Profesa Sospeter Muhongo, ameiomba Serikali kuanza mchakato wa kuipandisha Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini ili iwe wilaya kamili kwa maelezo kuwa halmashauri hiyo ina vigezo na sifa zote za kuwa wilaya.
Profesa Muhongo ametoa ombi hilo leo, Jumamosi, Julai 4, 2026, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Suguti na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.
Amesema endapo Serikali itaridhia ombi hilo, fedha za ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya zitatolewa na wakazi wa halmashauri hiyo na siyo kutegemea Serikali.
“Sisi siyo maskini, sisi ni wavuvi, wafugaji, wakulima na wachimba madini. Mkiridhia ombi letu la kuwa wilaya kamili, suala la ujenzi wa ofisi ya DC litakuwa juu yetu wenyewe na wala halitakuwa gharama za Serikali,” amesema.
Amefafanua kuwa halmashauri hiyo yenye kata 21 na vijiji 68 ina huduma za jamii katika maeneo yote, ikiwamo shule za msingi na sekondari, huku akieleza kuwa katika suala la elimu, kila kijiji kina wastani wa shule mbili za msingi, huku kukiwa na shule za sekondari 33, zikiwamo sita za kidato cha tano na sita.
Katika sekta ya afya, Profesa Muhongo amesema halmashauri hiyo ina hospitali ya halmashauri yenye vifaa vya kisasa, huku akiomba Serikali kutoa fedha za kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo ili hatimaye iweze kutoa huduma kikamilifu.
Amesema endapo eneo hilo litakuwa wilaya kamili, itasaidia kuchochea kwa kasi maendeleo ya halmashauri hiyo kwa masilahi ya wakazi wa jimbo hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesema halmashauri hiyo ni miongoni mwa halmashauri za mkoa huo zinazotekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati na kuzingatia ubora sambamba na thamani ya fedha.
Amesema ili kuchochea uchumi wa eneo hilo, ujenzi wa Barabara ya Musoma - Busekekela ni suala muhimu, hivyo kuomba Serikali kufanya utaratibu ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
“Barabara ni kikwazo kikubwa cha ukuaji wa uchumi katika eneo hili kwa sababu hapa miradi inatekelezwa kwa ubora na kwa kasi inayotakiwa. Naiomba Serikali itujengee hii barabara ili kuondokana na kero hii ya muda mrefu, na pia itasaidia kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii nzima,” amesema.
Akizungumza kuhusu ujenzi wa Barabara ya Musoma - Busekekela yenye urefu wa kilomita 92, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, amesema barabara hiyo itajengwa kwa awamu; ya kwanza itahusisha ujenzi wa kilomita 40 pamoja na Daraja la Suguti.
“Tuko katika hatua za mwisho, mkandarasi ameshapatikana na kama mambo yatakwenda vizuri, ujenzi utaanza mwezi ujao. Hivyo niwaondoe hofu wakazi wa Musoma Vijijini kuhusu barabara hii ambayo imekuwa kero kwa muda mrefu,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa halmashauri hiyo wamesema suala la halmashauri yao kuwa wilaya ni hitaji lao la muda mrefu, hivyo kuomba mchakato huo ufanyike kwa haraka ili kusogeza zaidi huduma kwa wananchi.
“Pamoja na kuwa tuna halmashauri huku, lakini zipo zile huduma ambazo tunazihitaji kutoka ofisi ya wilaya na, kutokana na umbali uliopo, wengi tunashindwa; inabidi tusubiri hadi ziara ya mkuu wa wilaya. Tukiwa na wilaya, mambo mengi yatarahisishwa,” amesema Elia Ekwabi.
Akizungumzia ombi la kuwa wilaya, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Festo Dugange, ameitaka halmashauri hiyo kufuata mchakato unaotakiwa ili kuwasilisha ombi hilo Tamisemi kwa hatua zaidi.
“Anzeni vikao vya vijiji, kata, kisha kamati za ushauri za wilaya na mkoa. Baada ya hapo maombi yaje Tamisemi kwa hatua nyingine,” amesema.
Kutokana na ombi hilo, Waziri Mkuu amesema halmashauri hiyo ina sifa za kupata wilaya kamili kutokana na idadi ya watu, namna miradi inavyotekelezwa na sifa nyingine, hivyo kutoa msisitizo kwa mamlaka husika kufanya mchakato ili kufikisha ombi hilo kwa mamlaka za juu kwa ajili ya uamuzi.
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amepiga marufuku hospitali zote za umma nchini kuwatoza fedha za mafuta wagonjwa wanaopata rufaa kutoka kituo kimoja cha kutolea huduma za afya kwenda kituo kingine.
Amesema lengo la Serikali kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya kwa kununua magari ya kubeba wagonjwa ni kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma za afya kwa haraka pasipo na kikwazo chochote.
Amesema suala la mafuta kwenye magari hayo ni jukumu la Serikali, hivyo kuwatoza wagonjwa gharama hizo ni kinyume cha utaratibu na kwamba yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua.
“Hawa watumishi hawajawahi kukosa mafuta wakiwa wanakwenda kwenye vikao na semina, lakini likija suala la wagonjwa mafuta yanakosekana. Sitaki kusikia jambo hili tena; atakayekwenda kinyume atachukuliwa hatua,” amesema.
Awali, kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara, Dk Mwigulu amezindua Shule Mpya ya Msingi Kasoma iliyojengwa kwa Sh336.9 milioni.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Palela Msongela, amesema shule hiyo itaanza kutoa huduma Julai 6, 2026, huku akieleza kuwa itasaidia kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu wanafunzi wanaotoka katika eneo hilo.
“Wanafunzi kutoka katika Kijiji cha Kaboni walikuwa wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita nane kwenda na kurudi shuleni. Sasa shule hii itawasaidia kuondokana na hali hiyo,” amesema.