Kero maji, barabara zatawala ziara ya Dk Mwigulu
Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba akiwa na baadhi ya viongozi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Butiama. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Kero hizo zimewasilishwa kwa njia mbalimbali, ikiwamo maandishi, michango ya wananchi katika mikutano hiyo na kupitia wabunge wa majimbo pamoja na wabunge wa viti maalumu
Butiama. Kero ya ukosefu wa huduma barabara, maji na ardhi zimejitokeza kwa wingi katika mikutano ya hadhara iliyofanywa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, wakati wa ziara yake katika halmashauri tano za Mkoa wa Mara.
Katika siku tatu ya ziara hiyo iliyoanza Julai mosi, 2026, Leo Ijumaa Julai 3, 2026, Dk Mwigulu amekagua na kuweka jiwe la msingi katika miradi mitatu ya maendeleo, sambamba na kufanya mikutano mitano ya hadhara yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Kero hizo zimewasilishwa kwa njia mbalimbali, ikiwamo maandishi, michango ya wananchi katika mikutano hiyo na kupitia wabunge wa majimbo pamoja na wabunge wa viti maalumu.
Miongoni mwa changamoto zilizojitokeza kwa wingi ni migogoro ya ardhi, katika kila mkutano kundi la wananchi wenye malalamiko hayo lilikuwa kubwa zaidi baada ya Waziri Mkuu kuwaelekeza wananchi kukaa katika makundi kulingana na aina ya changamoto walizonazo.
Mkazi wa Butiama, Ester Buruma amesema wilaya hiyo inakabiliwa na kero kubwa ya maji licha ya uwepo wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya zaidi ya Sh70.5 bilioni.
"Hapa hatuna maji, wananchi tunateseka sana ingawa kuna huo mradi mkubwa wa Mugango- Kiabakari, tunakuomba Waziri Mkuu utusaidie Butiama tupate maji tunateseka sana," amesema.
Mkazi wa Wilaya ya Serengeti, Ibrahim Chacha amesema wilaya yao haina mtandao wa barabara hali iliyofanya wilaya hiyo kutokuunganishwa na wilaya zingine za mkoa wa Mara.
"Wilaya yetu ni kitovu cha utalii lakini ndio wilaya ambayo haina barabara ya lami iwe ya kuunganisha wilaya na wilaya au hata zile za ndani ya mji kwa ujumla hali ya barabara zetu ni mbaya sana, Serikali tunaomba mfanye jambo," amesema.
Mbunge wa Serengeti, Mary Daniel amesema licha ya Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, jimbo hilo bado linakabiliwa na changamoto za barabara na maji.
Amesema baadhi ya barabara ziko katika hali mbaya kiasi cha kuathiri mawasiliano kati ya Serengeti na wilaya nyingine za Mkoa wa Mara.
Pia, ameomba Serikali kuanzisha mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo, akieleza kuwa chanzo cha sasa cha Bwawa la Manchira hakitoshelezi mahitaji ya wananchi.
Mbunge wa Rorya, Jafari Chege amesema jimbo hilo linahitaji maboresho ya barabara, upatikanaji wa majisafi na salama pamoja na umeme katika baadhi ya vitongoji.
Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, ameieleza Serikali kuwa wananchi wa jimbo hilo wanakabiliwa na changamoto za maji na ubovu wa barabara, akitaka zipatiwe ufumbuzi wa haraka.
Akijibu hoja hizo, Dk Mwigulu amesema baadhi ya miradi ya maendeleo, hususan ya barabara na maji, ilisimama kwa muda baada ya Serikali kuelekeza rasilimali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwamo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere.
Amesema kukamilika kwa baadhi ya miradi hiyo sasa kumeipa Serikali nafasi ya kuendelea na utekelezaji wa miradi iliyokuwa imesimama ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Pia, amesema Serikali imebadili utaratibu wa usimamizi wa fedha kwa kuelekeza mapato yanayokusanywa kwa ajili ya sekta mbalimbali kupelekwa moja kwa moja katika mifuko husika badala ya kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali.
"Fedha za barabara zitaenda moja kwa moja kwenye mfuko wa barabara; na za maji kwenye mfuko wa maji. Hii itasaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi," amesema.
Kuhusu Mkoa wa Mara, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuharakisha mchakato wa kutangaza zabuni za ujenzi wa baadhi ya barabara, akimtaka kukamilisha hatua hiyo ndani ya mwezi mmoja.
Amesema wananchi wasiwe na wasiwasi kwa kuwa Serikali itaendelea kutekeleza ahadi zote zilizotolewa, akibainisha kuwa utekelezaji wa bajeti ya kwanza ya ilani ya uchaguzi tayari umeanza.
Akiwa wilayani Butiama, Dk Mwigulu amesema wilaya hiyo inahitaji kupewa kipaumbele kutokana na kuwa mahali alipozaliwa na kuzikwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Kutokana na hali hiyo, ameiagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) kufanya tathmini ya gharama za ujenzi wa barabara za ndani za wilaya hiyo, huku Ruwasa ikitakiwa kuwasilisha tathmini ya miradi ya maji ndani ya mwezi mmoja.
Aidha, ameagiza kukamilishwa kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Butiama, akisema Serikali tayari imetoa Sh3.6 bilioni kwa mradi huo uliokamilika kwa zaidi ya asilimia 90, huku Sh500 milioni zikitengwa katika bajeti ya mwaka 2026/27 ili kuukamilisha.