CDF wa Kenya apata ajali ya helkopta, Ruto aitisha kikao cha dharura

Muktasari:

  • Rais William Ruto ameita Baraza la Usalama la Kitaifa (NSC) katika Ikulu ya Nairobi baada ya chopa ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kuanguka leo Alhamisi ya Aprili 18, 2024

Kenya. Hofu imetanda nchini Kenya baada ya helkopta ya jeshi iliyokuwa imembeba Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo (CDF), Jenerali Francis Ogolla kupata ajali leo Aprili 18, 2024.

Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Kenya, William Ruto ameitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Kitaifa (NSC) katika Ikulu ya Nairobi.

Taarifa iliyochapishwa katika Tovuti ya Nation ya Kenya leo imesema kikao hicho kinajumuisha, Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Ulinzi, Mwanasheria Mkuu, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi, na Inspekta Jenerali wa Polisi.

Wengine ni  Mwanasheria Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ujasusi (NIS), Inspekta Jenerali wa Polisi na Mshauri wa Usalama wa Kitaifa.

Tovuti hiyo imeeleza kuwa ajali hiyo imetokea katika mpaka wa Kaben-Cheptule kati ya Elgeyo Marakwet na Kaunti ya Pokot Magharibi na watu watano waliokuwamo pamoja na CDF Ogolla wamethibitka kufariki dunia huku watatu wakiwa mahututi.

Helikopta hiyo baada ya kuanguka iliwaka moto katika eneo la Sindar kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet.

Tovuti hiyo pia imeeleza kuwa, walionusurika wamekimbizwa hospitali na ndege nyingine ya Jeshi la KDF,  Kamanda wa Elgeyo Kaunti ya Marakwet Peter Mulinge amethibitisha tukio hilo

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa, kulikuwa na chopa tatu zilizokuwa zinaondoka katika eneo hilo na yenyewe ilikuwa ya kwanza kupaa kabla ya kuanguka dakika chache.

Kulingana na ripoti hizo, helikopta hiyo ilikuwa ikipaa kutoka Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Cheptuel.

Timu hiyo ilikuwa imeondoka kwenye mkutano uliokuwa umeitishwa kujadili hali ya usalama katika eneo la Pokot Magharibi na viongozi kadhaa wakuu walikuwepo.

Aidha, Tuko News imesema waliofariki dunia walikuwa wakifanya ziara ya kutathmini hali ya usalama na kujadili uwezekano wa kufunguliwa kwa shule katika eneo la mpaka kati ya Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet.

Hata hivyo, Msemaji wa Serikali ya Kenya, Isaac Mwaura amewataka Wakenya kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu.

"Ndugu Wakenya wenzangu, taarifa zaidi kuhusu ajali ya ndege ya kijeshi yatatolewa hivi karibuni. Tuepuke uvumi wowote katika wakati huu mgumu."

(Imeandaliwa na Sute Kamwelwe)