Idadi ya vifo tetemeko la ardhi Morocco yafikia 1,037

Muktasari:

  • Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco, imesema idadi ya vifo vitokanavyo na tetemeko la ardhi, lililotokea nchini Morocco Ijumaa usiku, imeongezeka ambapo watu 1,037 wamefariki huku wengine zaidi ya 1,200 wamejeruhiwa katika janga hilo.

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco, imesema idadi ya vifo vitokanavyo na tetemeko la ardhi, lililotokea nchini Morocco Ijumaa usiku, imeongezeka ambapo watu 1,037 wamefariki huku wengine zaidi ya 1,200 wamejeruhiwa katika janga hilo.

DW imeripoti kuwa tetemeko hilo lenye ukubwawa 6.8 kwenye kipimo cha Richter, limesababisha uharibifu wa majengo katika vijiji vya milima ya Atlas hadi kwenye mji wa kihistoria, Marrakech.

Imeelezwa kuwa wengi wa watu walipoteza maisha yao, wanatoka katika mikoa mitano iliyo karibu na eneo lililoathiriwa zaidi na tetemeko hilo, na kwamba idadi ya vifo na majeruhi inatarajiwa kuongezeka wakati waokoaji wakifukua vifusi vya majengo yaliyoanguka na wakijaribu kuyafikia maeneo yasiyofikika kwa urahisi.

Televisheni ya taifa hilo, imeonyesha watu wakiwa wamejazana katika mitaa ya Marrakech wakati wa usiku huku wakihofia kurejea kwenye majengo.

Katika mji huo, Msikiti maarufu wa Koutoubia uliojengwa karne ya 12, ambao mnara wake una urefu wa mita 69 umeharibiwa pia ingawa kiasi cha hasara bado hakijajulikana.

Mkuu wa mji wa Talat N'Yaaqoub, ulio karibu na kitovu cha tetemeko hilo Abderrahim Ait Daoud, aliiambia tovuti ya habari ya 2M ya Morocco kuwa, nyumba kadhaa zilianguka na kwamba huduma za umeme hazipatikani, huku baadhi ya barabara zikijifunga katika maeneo mengine.

N'Yaaqoub amesema kuwa mamlaka zinafanya kazi ili kusafisha barabara katika eneo la Al Haouz ili kuyaruhusu magari ya kubebea wagonjwa kupita na kupeleka misaada kwa waathiriwa.

Hata hivyo ameongeza kuwa, umbali mrefu kati ya vijiji vilivyo kwenye milima unamaanisha kuwa itachukua muda kufahamu kiwango cha uharibifu uliotokana na tetemeko hilo la ardhi.

Jeshi la Morocco na huduma za dharura wameratibu juhudi za kufikisha misaada katika maeneo yaliyopatwa na uharibifu.

Awali, vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa barabara zinazoelekea kwenye eneo la milima karibu na sehemu iliyoathiriwa zaidi na tetemeko hilo zilikuwa zimesongwa na magari, na zimezuiwa na miamba iliyoanguka na kuziziba hali inayopunguza kasi ya uokoaji.

Malori yaliyobeba mablanketi, makoti na taa yalikuwa yakielekea huko.

Dunia yaonesha mshikamano na Morocco kufuatia tetemeko

Wakati hali ikiwa hivyo nchini humo, baadhi ya viongozi wa mataifa mbalimbali duniani wametoa pole kufuatia janga hilo. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X ambao awali ulijulikana kama twitter ameandika kuwa "Ni habari mbaya kutoka Morocco. Tuko pamoja na waathiriwa wa tetemeko katika nyakati hizi ngumu". 

Shirika la Ujerumani la msaada wa kiufundi limesema linajiandaa kutoa msaada kama litahitajika kufanya hivyo.

Naye Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, wakati akifungua mkutano wa kilele wa mataifa yanayounda kundi la G20 unaofanyika New Delhi, amesema kuwa, wanawaombea nafuu ya haraka majeruhi waliotokana na tetemeko hilo la ardhi na kwamba wako tayari kutoa msaada unaohitajika.

Kwa upande wake, Rais wa Russia, Vladmir Putin, ametoa salamu za rambirambi kwa Mfalme wa Morocco, Mohammed VI, akisema kuwa nchi yake imeguswa na kuhuzunishwa na maafa hayo. Ametoa pole kwa familia na marafiki wa waathiriwa na kuwatakia nafuu ya haraka waliojeruhiwa.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, pia hakubaki nyumba, kwa ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa X kuwa "tunasimama na kaka zetu wa Morocco kwa kila namna katika siku hii ngumu."

Katika taarifa tofauti, wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki nayo imeandika kuwa Ankara, iko tayari kutoa msaada wa hali na mali kwa Morocco.

Vile vile, Rais wa Ufaransa Emannuel Macron, Joe Biden wa Marekani, Volodymyr Zelensky wa Ukraine, Kaimu waziri Mkuu wa Uhispania, na Waziri Mkuu wa Uswidi wametoa salamu za pole na kuonesha kusikitishwa kwao na tukio hilo.  Umoja wa Falme za Kiarabu na Taiwan, zimetoa pia ujumbe wa pole kufuatia tetemeko hilo