Israel yadai kumuua kamanda wa Hezbollah

Muktasari:

  • Kamanda huyo aitwaye Ali Ahmed Hussein wa kikosi cha wasomi cha Hezbollah cha Radwan Forces anadaiwa kuuawa na ndege za Israel katika eneo la Sultaniyeh kusini mwa Lebanon, jeshi limesema katika taarifa.

Jerusalem. Jeshi la Israel limesema limemuua kamanda wa kundi la Hezbollah katika shambulio la anga lililotekelezwa usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Aprili 8, 2024 huko nchini Lebanon.

 Kamanda huyo, Ali Ahmed Hussein wa kikosi cha wasomi cha Hezbollah cha Radwan Forces anadaiwa kuuawa na ndege za Israel katika eneo la Sultaniyeh kusini mwa Lebanon, jeshi limesema katika taarifa yake, huku likimtuhumu kwa mashambulizi dhidi ya Israel katika miezi ya hivi karibuni.

Shirika la Habari la AFP limeandika kwamba takriban watu wengine wawili wameuawa katika shambulizi hilo kwa mujibu wa jeshi la Israel na vyombo vya habari vya Serikali ya Lebanon.

Aidha, Jeshi limesema Kamanda Hussein alifanya mashambulizi mengi kuelekea eneo la Israel kutoka Lebanon tangu vita vilipozuka Oktoba 7, 2023 kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas ambao ni washirika wa Hezbollah.

Hezbollah, ambayo ina hazina kubwa ya makombora, imekuwa ikirushiana risasi mara kwa mara na vikosi vya Israeli tangu Hamas kutekeleza shambulio la Oktoba 7 dhidi ya Israeli, na kusababisha vita katika Ukanda wa Gaza.

Shambulio hilo lilisababisha vifo vya takriban watu 1,170, wengi wao wakiwa raia, lakini hadi sasa operesheni za kijeshi ya Israel ya kulipiza kisasi imeua takriban watu 33,175 huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya ya eneo linalotawaliwa na Hamas.