Rais Biden achoshwa na mauaji Gaza, amuonya Netanyahu

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Takwimu za mamlaka ya afya za Gaza zinaonyesha hadi sasa IDF imesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 30,800, wengi wao wakiwa wanawake na watoto tangu kikundi cha wapiganaji wa Hamas washambulie Israeli Oktoba 7, 2023 na kusababisha vifo vya Waisraeli 1,139.

Washington. Rais Joe Biden katika kuonyesha ameanza kuchoshwa na ongezeko la vifo Gaza, ameonya kwamba kuna mstari mwekundu ambao Israeli haitakiwi kuuvuka, huku akimshutumu Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu kwamba anachofanya kinaiumiza Israel badala ya kuisaidia.
Biden alitoa kauli hiyo kwenye mahojiano yake ya jana Jumamosi, Machi 9, 2024 na kituo cha televisheni cha MSNBC cha Marekani ambayo inaonyesha amechoshwa na ongezeko la vifo vya Wapalestina huko Gaza vinavyotokana na mashambulizi ya Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF).

New Content Item (1)
New Content Item (1)


Takwimu za mamlaka ya afya za Gaza zinaonyesha hadi sasa IDF imesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 30,800, wengi wao wakiwa wanawake na watoto tangu kikundi cha wapiganaji wa Hamas washambulie Israeli, Oktoba 7, 2023 na kusababisha vifo vya Waisraeli 1,139.
Msimamo wa Biden unaonekana kubadilika baada ya kauli yake ya Oktoba mwaka jana, mjini Tel Aviv, kuhusu shambulio la roketi kwenye Hospitali ya Ahli Arab lililosababisha vifo vya kati ya watu 200 hadi 300 huko Gaza, kwamba halikufanywa na Israel, bali limefanywa na timu nyingine.
Rais Biden pia alitumia mahojiano hayo na MSNBC aliyofanya siku chache baada ya kutoa hotuba ya hali ya kitaifa kwenye mkutano wa ‘The State of the Union’,  kujibu mapigo ya mpinzani wake wa kisiasa, Donald Trump ambaye siku za karibuni alimshutumu (Biden) kwa kuacha mauaji ya halaiki yaendelee kutokea Gaza. “Kinachoendelea Gaza si mauaji ya halaiki, ila watu wanaguswa na vifo hivyo,” alisema Biden.
“Wanachosema kinatokana na huzuni yao kuhusu mauaji ya Gaza, siwalaumu kwa kuwa na huzuni, kuna familia kule, kuna watu wanakufa. Wanataka kitu kifanyike na wanasema Joe, fanya kitu, fanya kitu. Lakini, wanachofikiria wao ni mauaji ya halaiki, wakati siyo sahihi, ni kitu kingine tofauti,” alisema Biden.
Alisema mpango wa Israel wa kuushambulia mji wa Rafah ambao ndio eneo pekee Wapalestina wamekimbilia huko kukwepa mashambuizi ya IDF, itakuwa kuvuka mstari mwekundu kwa Waziri Mkuu, Netanyahu, lakini hatoiacha Israel. Zaidi ya Wapalestina 2.3 milioni wamekimbilia mji wa Rafah.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

 “Ninamfahamu Bibi kwa miaka 50 (Bibi ni jina la utani la Netanyahu). Israel ina haki ya kujiinda kutokana na mashambullizi ya Hamas, lakini Netanyahu lazima, lazima, lazima awe mwangalifu kuzuia madhara kwa raia Gaza,” alisema Biden na kuongeza: “Anaiumiza Israel badala ya kuisaidia kwa kuua raia. Hili ni kosa,” alisema Biden.
“Lakini, kuna mstari mwekundu kama atauvuka…,” alisema Biden bila kumalizia itakuwaje huo mstari ukivukwa na kungeza kuwa utawala wake hauwezi kuvumilia vifo vya Wapalestina zaidi 30,000.
Biden alimuonya Netanyahu kwamba asiifanye Gaza kama Marekani ilivyoivamia Irag na Afghanistan (japokuwa mwanzoni alikosea na kuitaja Ukraine kwamba ndio Afghanistan).
“Haikuwa lazima, haikuwa lazima. Hii ilisababisha matatizo zaidi ya kuyaondoa, zaidi ya kuyatibu,” alisema Biden kuhusiana na matatizo yaliyotokea baada uvamizi wa Marekani katika nchi za Iraq na Afghanistan.
Alisema Israel haitakiwi kuuvamia mji wa Rafah hadi iweke utaratibu wa kuwaokoa raia wasio na hatia waliokimbilia huko.
Biden alipoulizwa kuhusu mpango wake wa kusimamisha mapigano kama utafanyika kabla ya Waislamu kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, alijibu hilo linawezekana na hajakata tamaa.
Alisema kwa siku za karibuni alifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu ikiwamo Saudi Arabia na wote wako tayari kulegeza misimamo yao kwa Israel.
Biden alisema anatarajia kwenda Israel kwa mara nyingine na atahutubia Bunge la Israel ‘Knesset’ na kuzungumza na wananchi.

Netanyahu ni nani?
Netanyahu aliyezaliwa Tel Aviv mwaka 1946 kwa mara ya kwanza alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Israel mwaka 1996, akiwa na umri wa miaka 46 na aliitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 1999.
Komando huyo wa jeshi ambaye wafuasi wake walimpachika jina la "Mfalme Bibi" lenye maana ya "mtenda miujiza" kwa ustadi wake wa kushinda uchaguzi, mara ya pili alishinda uchaguzi na kuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo mwaka 2009 hadi mwaka 2021.
Alishiriki katika uvamizi wa uwanja wa ndege wa Beirut mwaka 1968 na kupigana vita mwaka 1973 vya Mashariki ya Kati.

Alivyoingia kwenye siasa

Mauaji ya kaka yake Luteni Kanali Jonathan Netanyahu aliyekuwa mmoja wa makomando waliotumwa kwenda Entebbe nchini Uganda kuwaokoa mateka wa Israel ndicho kilichomuingiza kwenye siasa.
Jonatahn mwaka 1976 alikuwa kwenye uvamizi huo wa Entebbe uliopewa majina ya Kiingereza ya ‘Operation Entebbe’ au ‘The Entebbe Raid’ na ‘Operation Thunderbolt’, makomando watano wa Isarel walijeruhiwa na mmoja ambaye ni Jonathan alikufa.
Ndege ya Israel ilibeba makomando 100 kwenda Entebbe nchini Uganda kuwaokoa mateka 106 na walitumia dakika 90 kukamilisha uvamizi huo. Hata hivyo, mateka 102 waliokolewa na watatu waliuawa.
Kifo cha Jonatahn kilileta athari kwenye familia ya Netanyahau na jina lake likaanza kujulikana sana Israel.
Netanyahu alianzisha taasisi ya kukabiliana na ugaidi kama kumbukumbu ya kaka yake na mwaka 1982 akawa naibu mkuu wa Israel katika ujumbe uliokuwa Washington, nchini Marekani.

Maisha ya kisiasa

Netanyahu baada ya kuingia kwenye siasa akiwa mzungumzaji mzuri wa lugha ya Kiingereza mwenye lahaja ya Marekani, akawa mtu maarufu katika vituo vya runinga vya Marekani na mtetezi wa kutegemewa wa Israel.
Pia, alichaguliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Israel katika Umoja wa Mataifa huko New York mwaka 1984.

Aliyoyafanya akiwa Waziri Mkuu

Netanyahu alipokuwa Waziri Mkuu kwa mara ya pili alikubali kusitisha ujenzi wa makazi katika ukingo wa magharibi kwa miezi 10 kitu ambacho hakikuwa kimewahi kutokea na kuwezesha mazungumzo ya amani na Palestina, lakini majadiliano hayo yakagonga mwamba mwishoni mwa mwaka 2010.
Ingawa mwaka 2009 alikuwa ametangaza kukubali uwepo wa eneo la Palestina mkabala na Israel kwa masharti, baadaye alibadilisha msimamo.
"Eneo la Palestina halitaundwa, sio kama watu wanavyolizungumzia hili. Halitawahi kutokea," aliambia kituo cha habari cha Israeli mwaka 2019.

Kukabiliwa na mashtaka

Mwaka 2016, Netanyahu alikabiliwa na uchunguzi wa madai ya ufisadi, ulaghai na ukiukaji wa uaminifu katika kesi tatu tofauti Novemba 2019.
Netanyahu alidaiwa kukubali zawadi kutoka kwa mfanyabiashara tajiri aliyetaka kupewa upendeleo.
Hata hivyo, Netanyahu alikanusha madai hayo na kusema kwamba yanachochewa kisiasa na wapinzani wake.
Alifunguliwa mashtaka hayo Mei 2020, na kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Israel kukabiliwa na kesi za aina hiyo, hata hivyo aligoma kujiuzulu.
Imeandikwa na Noor Shija