Joe Biden afanya ziara ya kushtukiza Ukraine
Rais wa Marekani, Joe Biden (kushoto) akifanya mazungumzo na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky (Kulia).
Muktasari:
- Rais wa Marekani, Joe Biden Jumatatu amefanya ziara katika mji mkuu wa Kyiv,i Ukraine ikiwa ni mara ya kwanza tangu uvamizi wa Urusi nchini humo.
Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Joe Biden amefanya ziara katika mji mkuu wa Kyiv, Ukraine ikiwa ni siku chache kabla ya maadhimisho ya mwaka mmoja wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Biden amefanya ziara hiyo leo Jumatatu, Februari 20, 2023 ikiwa ni ya usiri mkubwa baada ya kuwasili bila taarifa.
"Joe Biden, karibu Kyiv! Ziara yako ni ishara muhimu sana ya kuungwa mkono na wananchi wote wa Ukraine," Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy ameandika kwenye mtandao wa kijamii akimkaribisha Biden.
Kwa mujibu wa DW, ziara hiyo ambayo haikuwa imetangazwa kwa sababu za kiusalama, imekuwa ni safari ya kwanza ya Biden nchini Ukraine tangu Urusi ilipoanzisha vita hivyo.
Katika hotuba yake ya pamoja kwa waandishi wa habari, Zelenskyy amesema mazungumzo na Biden yanaileta Ukraine karibu na ushindi, huku Rais wa Marekani akiahidi kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine.
"Leo mazungumzo yetu yalikuwa na matunda mengi yalikuwa muhimu sana,”amesema Zelenskyy.
Ziara ya ghafla ya Biden huko Kyiv imedumu kwa karibu saa tano, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.