Kimbunga kutikisa tena Msumbiji
Muktasari:
- Kimbunga Freddy ambacho kiliikumba Madagascar na Msumbiji mwezi uliopita na kuleta maafa yakiwemo mafuriko, kinatarajiwa kurejea tena nchini Msumbiji.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Msumbiji imesema Kimbunga Freddy kinatarajiwa kurejea katika nchini humo huku mikoa ya Zambézia na Sofala ikiwa ni maeneo yanayomulikwa zaidi kuathiriwa, kulingana na makadirio ya mamlaka.
Kwa mujibu wa wataalamu wa hali ya hewa, dhoruba hiyo, inakwenda kwa kasi ya kilomita 13 kwa saa kuelekea pwani ya kusini magharibi mwa Madagascar, na inaweza kufikia hatua ya dhoruba kali ya kitropiki siku leo Jumatatu.
Taasisi ya Kitaifa ya Hali ya Hewa ya Msumbiji imetabiri kuendelea kunyesha kwa mvua kubwa zaidi ya 200mm kwa saa 24 usawa wa bahari na upepo wa hadi kilomita 110 kwa saa ambayo inaweza kuvuruga mawimbi ya baharini.
Shirika hilo limewaonya watu kuchukua hatua za tahadhari na usalama.
Takriban watu 7 wamefariki dunia kufuatia athari za kimbunga hicho huku Zaidi ya watu 11,500 wakiyaacha makazi yao na majengo 2,267 kuharibiwa.