Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kimbunga: Rais Malawi atangaza hali ya hatari

Lilongwe. Kufuatia uharibifu uliosababishwa na athari za Kimbunga Freddy ambacho kimesababisha maelfu kukosa makazi hadi kufikia Jumatatu jioni huku wengi wakipotea na kujeruhiwa, Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera ametangaza hali ya hatari katika wilaya 10 za kusini zilizoathirika.

Maeneo yaliyoathirika ni Jiji la Blantyre na wilaya zake za Chikwawa, Chiradzulu, Mulanje, Mwanza, Neno, Nsanje, Thyolo, Phalombe na Zomba.
Tangazo kwa umma kutoka kwa Katibu wa Rais na Baraza la Mawaziri, Colleen Zamba lilisema Chakwera ametoa tamko la hatari kwa mujibu wa kifungu cha 32 (1) cha Sheria ya Maandalizi na Misaada ya Maafa Sura ya 33:05 ya Sheria za Malawi.

Zamba aliuhakikishia umma kwamba Serikali tayari inashughulikia suala hilo, ikitoa msaada wa haraka kwa wilaya zote zilizoathirika na kuomba msaada wa ndani na wa kimataifa kwa familia zote zilizoathiriwa na janga hilo.


Idadi ya vifo yaongezeka
Idadi ya vifo nchini humo imeongezeka maradufu hadi kufikia 100 Jumatatu, huku 85 vikirekodiwa katika jiji la Blantyre pekee, mamlaka imesema.
Nchi inajitahidi kuzuia athari za kimbunga, ambacho kimesababisha uharibifu hasa katika wilaya hizo.

Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali imeharibu nyumba, barabara na madaraja na kusomba mazao mashambani huku huduma za kijamii zikivurugika.
Hospitali kuu ya rufaa mjini Blantyre ilisema imeelemewa na idadi kubwa ya miili inayopokea.

Aidha hospitali hiyo ilitoa wito kwa familia zilizofiwa au ambazo ndugu zao wamepotea, kwenda hospitali kutambua na kuchukua miili kwa ajili ya mazishi kwa kuwa haina nafasi.
Kimbunga hicho kimeathiri uwezo wa kuzalisha umeme huku sehemu nyingi zikikabiliwa na kukatika kwa umeme kwa muda mrefu.

Kampuni ya kitaifa ya kuzalisha umeme inasema haiwezi kurejesha nguvu kwa mtambo wake wa kufua umeme kutokana na mrundikano wa takataka uliosababishwa na mafuriko.
Kwa mujibu wa BBC, wataalamu wa hali ya hewa wanasema mvua kubwa na mafuriko yataendelea, huku kimbunga hicho kikitarajiwa kuanza kuondoka Malawi kurejea Bahari ya Hindi leo Jumatano.


Mwitikio wa misaada
Kundi la wakazi wa Blantyre linalojulikana kama Malawi Land Rover Defender Club, lilitangaza kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba limeanza juhudi za uokoaji kwa watu ambao wameathiriwa pakubwa na maafa yaliyosababishwa na kimbunga hicho.

Hadi kufikia Jumatatu jioni, wajumbe wa kundi hilo walikuwa Chibowa, jamii inayopakana na Chilobwe na Manja, wakiwahamisha waathirika na mali zao kwenda kwenye makazi ya muda ambayo Serikali imeyaanzisha huko Manja.

“Hali ni mbaya na tunaomba msaada zaidi wakati tukiendelea na juhudi za kuwasaidia wenzetu wenye mahitaji,” alisema mmoja wa wajumbe wa kundi hilo.
“Tutakuwa Chichiri Shopping Mall kesho asubuhi kukusanya bidhaa na vyakula ambavyo vitasaidia kupunguza hali ya watu walioathirika,” aliongeza.