Kupindupindu chazidi kuua Malawi, wengine wagoma kutibiwa

Muktasari:

  • Idadi ya vifo inayotokana na kipindupindu imezidi kuongezeka nchini Malawi na idadi ya watu imefikia 1,000.

Malawi. Ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea tangu Machi 2022 nchini Malawi, umeua zaidi ya watu 1,000 na Wizara ya Afya imetangaza leo Jumatano kukosekana chanjo ya ugonjwa huo, huku baadhi ya watu wakigoma kutibiwa kutokana na imani za dini zao.

 Idadi ya vifo ilifikia 1,002 siku ya Jumanne, na kufanya mlipuko wa sasa wa kipindupindu kuongezeka zaidi kwenye nchi hiyo iliyoko kusini mwa Afrika.
Shirika la Habari la RFI limeripoti kuwa, jumla ya watu 30,600 wameambukizwa tangu kesi za kwanza kuonekana mwaka jana.
Kipindupindu huambukizwa kwa kunywa maji au kula chakula kilichoambukizwa na bakteria. Kawaida husababisha kuhara na kutapika na inaweza kuwa hatari kwa watoto wadogo.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Adrian Chikumbe siku ya Jumanne aliliambia Shirika la Habari la AFP kuwa, “Kufikia mwezi Novemba, tulikuwa tumepokea karibu dozi milioni tatu za chanjo ya kumeza kutoka kwa Umoja wa Mataifa, lakini tulitumia chanjo zote tulizokuwa nazo."
Anaendelea kusema, "Ukweli kwamba kuna kampuni moja tu inayotengeneza chanjo ya kipindupindu duniani na hali hii inafanya kuwa vigumu kupata dawa hiyo, tunashindania chanjo sawa na kila mtu.”
Chikumbe ameongeza kuwa kuna sehemu ya wakazi wa Malawi wanakataa matibabu kwa kuzingatia imani za kidini, jambo ambalo linachangia kuenea kwa ugonjwa huo.
Septemba mwaka jana, WHO iliripoti kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa kipindupindu ulimwenguni, baada ya kupungua kwa miaka kadhaa.
Mabadiliko ya hali ya hewa yanatajwa kuwa mojawapo ya sababu pamoja umaskini.

Ugonjwa huu huathiri kati ya watu milioni 1.3 na milioni 4 duniani kila mwaka, na kusababisha vifo vya hadi watu 143,000.