Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hekaya za Mlevi: Soka sasa si burudani ila dimbwi la kubeti

Muktasari:

  • Kila mmoja anajua utamu wa kuku wa kienyeji, lakini anapozalishwa na kufugwa kizungu anapoteza ladha.

Dar es Salaam. Waswahili husema “kuchamba kwingi...” au labda nitumie tafsida: “kuoga kwingi kutoka na uchafu”. Hata mboga ukiipika zaidi ya kiwango cha mapishi, utatoka na msosi ambao hata mdudu ataukataa. Ufundi unapozidi ladha inapungua, na hatimaye kwisha kabisa. 

Kila mmoja anajua utamu wa kuku wa kienyeji, lakini anapozalishwa na kufugwa kizungu anapoteza ladha.

Mpira wa miguu ulianza kama burudani kutokana na ufundi wa wachezaji. Kila mchezaji alitumia umbo lake kiufundi kutekeleza majukumu aliyopewa na timu yake. Kwa mfano walinda milango walikuwa wepesi wa kusafiri angani kuokoa mikwaju. Mabeki hasa wa kati walikuwa warefu na wenye kuhimili mikiki. Mifano yake ilikuwa Mohamed Bakari “Tall”, Jellah Mtagwa na wengineo. 

Ngoma ilianza kwa kipa kumrushia beki mbili, akapiga ndefu kwa namba saba, saba akamimina krosi ambayo ingemkuta namba tisa apige mkwaju au namba kumi afunge kwa kichwa. Ama kipa angeanza na beki tatu, angeisukuma kwa namba kumi na moja, naye angeingiza kati.

Mawinga wote walikuwa na mbio za kuwapita mabeki wa pembeni na kuingiza mpira kati kwa wafungaji.

Iwapo timu ingeshindwa kupata matokeo kwa kupitia pembeni, ingemtumia kiungo wa kati kuipenya ngome na kugawa mipira kwa wafungaji.

Hawa waliweza kufungua kuta za mabeki kwa uwezo wao wa kupiga chenga. Hapa nchini tulikuwa na Nico Njohole wa Simba na Adolf Rishard wa Pan. Yaani we acha tu, ungeweza hata kuishangilia timu pinzani kama imejipanga vizuri.

Wapenda kabumbu tulikuwa tukipata burudani isiyo na kipimo. Katika matukio ninayoyakumbuka vizuri, Pan walipopata kona walimtuma Jaffar Abdulrahman. Halafu washambuliaji vipisi vya watu kama Peter Tino walisimama kama hatua kumi kutoka alipo mlinda mlango. 

Wakamwelekeza Jaffar aulete mpira kwa kipa. Sasa hapo ungemwona golikipa jinsi alivyohaha; alijua atakapoudaka, kundi lote lile lingemvaa na kuingia naye nyavuni.

Lakini sasa ukimgusa tu golikipa, refa anaweza kukupa kadi ya njano. Si golikipa tu, hata mastaa kama Ronaldo na Messi wanalindwa vivyo hivyo. Zile enzi za Adam Sabu kukanyaga miguu ya Pondamali ili asiirukie kona zikaisha, sasa kuna sheria karibuni ishirini zinazoulinda mchezo huu.

Lakini hili sio linaloniumiza sana. Ila tumekuwa tukishuhudia kifo cha mchezo huu hatua kwa hatua, na sasa tunaelekea tamati ya mchezo wetu pendwa.

Wengi tuliowahi kuliona kandanda la akina Pele, Maradona na Zidane tunakubaliana kuwa hivi sasa tumeishiwa na hatuna maajabu tena katika soka.

Kwanza wachezaji walizuiwa kutumia vipaji vyao halisi mchezoni. Kocha anataka mchezaji asibaki na mpira hata kwa sekunde chache.

Ile jeuri ya Maradona kuipiga chenga timu pinzani kuanzia washambuliaji mpaka kipa imekwenda na maji. Na kwa sababu makocha wetu wanatoka Ulaya, basi Waafrika tunalazimika kucheza mpira wa Ulaya. Sijui akina Roger Miller wangefanyaje. 

Mbaya zaidi, wameanzisha vipimo vya kisayansi vya Uhalisia Pepe (Virtual Reality) kwa wachezaji. Vipimo hivi hutathmini kasi ya kufanya maamuzi ya haraka, uwezo wa kusoma mchezo, na utambuzi wa nafasi uwanjani. 

Mchezaji anapimwa jinsi anavyoweza kufanya maamuzi sahihi na ya haraka ndani ya sekunde chache. Nadhani “Goli la Mungu” la Maradona lingefutwa kabla ya kufungwa. 

Programu kama “Be Your Best” zinawawezesha wachezaji kushiriki matukio ya mechi wakiwa wamevalia miwani maalum. Hii inawapa uwezo wa kufanya mazoezi ya ubongo na kufuatilia takwimu za utambuzi.

Mifumo ya Vienna Test System hutumika kupima utayari wa mchezaji kukabiliana na msongo wa mawazo na kutathmini jinsi anavyoweza kujibu matukio ya haraka uwanjani.

Vifaa na programu kama vile NeurOlympics au S2 Cognition hutumika kupima kumbukumbu na wepesi wa kisaikolojia.

Husaidia kuelewa nyakati ambazo mchezaji amechoka kiakili, uwezo wa kukabiliana na presha na kubaini wachezaji wanaoweza kutulia na kutekeleza maelekezo ya mbinu (tactics) za mwalimu hata wanapokuwa wanashambuliwa vikali.

Sasa kuna hatari ya mchezo huu kuchezwa na roboti. Au pengine utachezwa kama gemu za kompyuta, na kuwekezwa zaidi kwenye kamari badala ya ufundi. 

Huku tunapoenda tutakuta refa anasetiwa, mchezaji anasetiwa, mechi inasetiwa, mpira umesetiwa, uwanja unasetiwa… Jamani, supu yake ndimu, mbona mwaitia nazi?

Na hapo ndipo ninapokumbuka msemo kwamba kufikiri kupita kiasi kunaweza kuharibu hata jambo ambalo mtu analijua vizuri.

Mchezaji akianza kupima kila hatua, kila pasi na kila mwelekeo kabla hajaugusa mpira, mara nyingi hupoteza kitu muhimu zaidi kuliko takwimu zote; silika yake. Ndiyo maana wakati mwingine unamwona mtoto wa mtaani akifanya chenga ambazo mchezaji wa kulipwa hawezi kuzifanya. 

Sio siri, Kombe la Dunia la mwaka 2026 limenichefua kinoma. Eti hata mpira wenyewe (namaanisha lile lililokuwa gozi la ng’ombe) umewekewa teknolojia ya vihisishi vinavyotuma taarifa kwa mfumo wa waamuzi. 

Sasa watakuja kwenye njumu na jezi, halafu kwenye viti vya uwanja. Bila shaka hilo lina manufaa katika kutafuta haki ya mchezo. Lakini swali linabaki: je, kila kitu kinapopimwa na kila uamuzi unasaidiwa na mashine, bado tunabaki na ule mchezo uliotufanya tuupende?