Mafuriko yafunga Uwanja wa Ndege Dubai, kiwango cha mvua kikiweka historia

Magari yakiendeshwa kwenye barabara iliyojaa maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Dubai mapema Aprili 17, 2024. Picha na AFP

Muktasari:

  • Wastani kwa mwaka Dubai hushuhudia milimita 94.7 au inchi 3.73 za mvua, sasa zimefikia milimita 142.

Dubai. Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha tangu Jumatatu Aprili 15, 2024 zimesababisha Uwanja wa Ndege wa Dubai kujaa maji na kufungwa kwa muda.

Shirika la habari la Serikali ya Dubai (WAM) katika taarifa yake limeeleza mvua hiyo kuwa tukio la kihistoria la hali ya hewa. Mvua hiyo ni kubwa kuliko kiwango kilichowahi kurekodiwa.


Picha ikimuonyesha mwanaume akipita kwenye barabara iliyofurika maji huko Dubai mnamo Aprili 16, 2024. Picha na AFP


Kwa mujibu wa Shirika la Habari la CNN, wastani wa mvua iliyonyesha kwa siku moja ni sawa na ya mwaka nzima katika nchi hiyo, iliyopo katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha Uwanja wa Ndege wa Dubai uliotangazwa hivi karibuni kuwa uwanja wa ndege wa pili kwa shughuli nyingi zaidi duniani, umejaa maji mithili ya bwawa.

Hali hiyo imesababisha usumbufu katika utekelezaji wa shughuli uwanjani hapo, huku mashirika mengi ya ndege yakiripoti kuchelewa kwa safari.


Teksi ikipita kwenye barabara iliyofurika kufuatia mvua kubwa iliyonyesha jijini Dubai mapema Aprili 17, 2024.  AFP


Shirika la Ndege la Flydubai limeahirisha safari zote hadi saa nne asubuhi ya leo Jumatano, Aprili 17, 2024.

Tovuti ya The Guardian imeripoti mvua zimenyesha kwa kiwango kikubwa zaidi katika kipindi cha miaka 75 iliyopita.

Mbali na Dubai, mvua kubwa imenyesha katika maeneo mengine ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), shirikisho la falme saba za Abu Dhabi, Dubai, Sharjah, Ajman, Umm Al Quwain, Ras Al Khaimah na Fujairah.

“Mvua zilianza Jumatatu usiku na kufikia Jumanne jioni, zaidi ya milimita 142 (inchi 5.59) zilikuwa zimelowesha jiji la jangwani la Dubai.

Kwa kawaida kiwango cha wastani kilichopo kwa mwaka mmoja na nusu ni milimita 94.7 au inchi 3.73 za mvua.

Inaelezwa kutokana na mvua hizo nyumba zimekumbwa na mafuriko na magari yalitelekezwa barabarani, huku mamlaka za Dubai zikichukua hatua ya kuondoa maji kwenye barabara.


Abiria wakisubiri safari zao za ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai leo Aprili 17, 2024. Ndege nyingi zilizokuwa zikiingia mnamo Aprili 16 zilizhirisha safari hadi leo asubuhi kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha. AFP


Kupitia ukurasa wa X, Kituo cha Kitaifa cha Hali ya Hewa kimewataka wakazi kuchukua tahadhari na kukaa mbali na maeneo yenye mafuriko.

Katika hatua nyingine, shule zimefungwa kuanzia jana Jumanne Aprili 16, 2024 hadi leo.

Msemaji wa uwanja wa ndege, amenukuliwa na Shirika la Habari la Gulf akisema safari zitahamishiwa kwenye viwanja vya ndege vilivyo jirani.

Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mashirika ya habari ya kimataifa