TMA yatoa angalizo la mvua mikoa mitano

Muktasari:

  • Wakati mvua ikiwapa biashara wachuuzi kwenye vijiwe vya kahawa, abiria walalama adha ya usafiri.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya hali mbaya ya hewa inayoweza kujitokeza kwa siku tano na kuathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi.

 Taarifa iliyotolewa na TMA leo Alhamisi Aprili 4, 2024 imetoa angalizo hilo kwa maeneo machache ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Morogoro, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia; Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba.

“Angalizo la mvua kubwa limetolewa katika maeneo machache ya mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi na Mtwara,” imesema taarifa hiyo.

Tahadhari hiyo imetolewa mvua ikiwa inaendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo mkoani Dar es Salaam kuanzia jana Jumatano Aprili 3, 2024.

Kwa mujibu wa taarifa ya TMA, mvua inatarajiwa kuendelea hadi Aprili 8, 2024 huku ikieleza uwezekano wa kutokea kwa hali hiyo ni wastani.

Mamlaka imesema kiwango cha athari zinazoweza kujitokeza ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji na kuathiri baadhi ya shughui za kiuchumi, ikiwataka wananchi kuzingatia tahadhari hiyo na kujiandaa.

Joachim Simon, mkazi wa Mwananyamala Msisiri ambaye makazi yake yamekuwa yakiathiriwa na mafuriko mvua kubwa zinaponyesha, amesema ni jambo jema TMA kutoa tahadhari mapema.

“Tunajua kipindi hiki ni cha mvua na maeno tunayokaa maji hujaa, ni vizuri taarifa imetolewa ili tuchukue tahadhari,” amesema Simon.

Mkazi wa Magomeni Suna, Hilda Salum amesema kila inapotolewa tahadhari wao wamekuwa wakizingatia kulingana na hali ya mvua kwa kuwa zipo zinazonyesha, lakini zisilete madhara kwao.

“Huwa tunazingatia tahadhari kulingana na hali ya hewa, mfano leo mvua imenyesha kwa muda mrefu, lakini haina madhara kwa kuwa hakuna maeneo yaliyojaa maji labda ikiendelea mfululizo kwa siku kadhaa,” amesema.

Februari 22, 2024 TMA ilipotoa taarifa ya uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za masika katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2024 ilishauri mamlaka na idara ya menejimenti ya maafa nchini kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.

TMA ilitoa tahadhari ikieleza vipindi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, hivyo kusababisha uharibifu wa miundombinu, mazingira, upotevu wa mali na maisha.

Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Ladislaus Chang'a alisema wakati huo kuwa kutakuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani kwa msimu wa masika, 2024 katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Ongezeko la mvua lilitarajiwa kuwa Machi.

Dk Chang’a alisema mvua za masika zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu na ya nne ya Mei, 2024 katika maeneo mengi.

Hali Dar es Salaam

Mvua inayoendelea kunyesha imesababisha adha ya usafiri kwa baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam, huku wengine wakilazimika kufanya biashara katika mazingira magumu, hususan kwenye maeneo ya wazi.

Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Gongo la Mboto wanaotumia Barabara ya Nyerere kutokana na mvua inayoendela kunyesha wanakabiliwa na adha ya usafiri inayochangiwa na ujenzi unaoendelea wa mradi wa mabasi ya mwendo wa haraka.

Wafanyabiashara kando mwa barabara katika maeneo ya Mombasa na abiria vituoni wanalazimika kukanyaga tope, huku kukiwa na maeneo yenye madimbwi makubwa ya maji.

Kutokana na adha hiyo, baadhi ya abiria hulazimika kutumia usafiri wa pikipiki au bajaji kufika wanakoelekea kutokana na daladala zinazotoa huduma kuwa chache.

Baadhi ya wenye magari binafsi wamekuwa wakibeba abiria katika njia hiyo wakiwatoza kati ya Sh2,000 na Sh3,000.

Wakati maeneo hayo hali ikiwa hivyo, baadhi ya maeneo ya barabara ya Kigogo kuelekea Jangwani yamejaa maji, hivyo kusababisha msongamano wa magari.

Bila kujali hali hiyo, wapo makuli walioendelea na kazi ya kupakia mizigo kwenye malori eneo la Jangwani.

Licha ya Barabara ya Mandela kuwa na foleni hata pasipokuwa na mvua, leo imekuwa kubwa zaidi ikichangiwa na mvua inayoendelea kunyesha.

Vijiwe vya kahawa

Wakati mvua ikiwaathiri wachuuzi wa vinywaji baridi kama vile soda, juisi na mtindi, wauza kahawa, tangawizi na mahindi ya kuchoma kwao ni neema wakipata wateja zaidi.

Mchuuzi wa kahawa eneo la Tabata Relini, Idd Rajab amesema msimu wa mvua ni mzuri kwake, kwani huuza zaidi kahawa, tangawizi, karanga au kashata.

Amesema wakati wa jua mara nyingi hufanya biashara kuanzi saa 11.00 alfajiri hadi saa nne asubuhi kutokana na joto au jua hulazimika kufunga biashara hadi saa 10.00 jioni ndipo afungue tena.

“Hiki ndicho kipindi chetu cha kufanya biashara, wateja ni wachache kutokana na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, vinginevyo kwa hali hii ya mvua wateja ni wengi,” amesema Idd.

Amesema kutokana na hali ya ubaridi unaotokana na mvua, kahawa na tangawizi huwaongezea joto mwilini wateja, huku wengine hufuata joto litokanalo na jiko.

“Kadri mteja atakavyokaa ndivyo tunavyozidi kufanya biashara, kama alikuwa anakaa saa mbili kunywa vikombe vitano anaweza kukaa saa sita na akanywa vikombe zaidi ya 15,” amesema.

Stanling Mshumbusi, aliyekuwa akinywa kahawa amesema kutokana na hali ya hewa ya baridi, akitumia kinywaji hicho huhisi joto mwilini.

“Mvua inaponyesha nikikosa hindi la kuchoma, utanikuta kijiwe chochote cha kahawa,” amesema.

Usafiri wa bodaboda

Dereva wa bodaboda mkazi wa Tabata, Rojas Maliki amesema kipindi cha mvua biashara huwa ngumu, kwani hukosa abiria na miundombinu ya barabara huharibika.

Maliki anasema wanawake wengi wakati wa mvua hawapandi bodaboda wakikwepa wasilowe.

“Kipindi cha mvua huwa hakuna kazi, biashara inakuwa ngumu hasa ukizingatia barabara huharibika, madaraja nayo hujaa maji, lakini kubwa zaidi vyombo vyetu vya usafiri vinaharibika na kusababisha tutumie gharama kubwa kuvitengeneza,” amesema Maliki.