Mafuriko yasomba Mjamzito na watoto wake

Mahali ambapo mafuriko yametokea na kuisomba nyumba aliyokuwa anaishi mjamzito na watoto wake

Muktasari:

  • Mjamzito na watoto wake watatu wanasadikiwa wamefariki dunia kufuatia mafuriko makubwa yaliyosomba nyumba yao walimokuwa wanaishi nchini Kenya.

Kenya. Mjamzito aliyetambuliwa kwa jina la Sabina Mwamidi pamoja na watoto wake watatu wnasadikiwa kufariki dunia baada ya nyumba yao kusombwa na mafuriko katika eneo la Mwatate nchini hapa.

Kwa mujibu wa mtandao wa TUKO, miili ya mama na watoto hao bado haijapatikana tangu mkasa huo ulipotokea Jumapili Aprili 2, 2023 kufuatia mvua kubwa iliyokuwa inanyesha na kusababisha mafuriko yaliyoezua nyumba ya Sabina.

Kamishna Msaidizi wa eneo hilo, Margaret Mwaniki almehibitisha kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha na kusema kuwa nyumba hiyo ilijengwa kando ya mto uliokauka.

Mwaniki aliyezungumza na mtandao huo, amesema kutokana na maelezo ya mashahidi, Mama huyo alikataa kutoka nyumbani kwake wakati mafuriko yanatokea na badala yake alijifungia ndani.

"Amekaa karibu na mto ambao huwa ni mto kawaida. Maji yalipokuja wenzake wakatoka wale majirani wanamwambia lakini yeye akarudi ndani akajifungia. Sasa ndio wakabebwa na maji pamoja na watoto," alisema Mwaniki.

Mbunge wa eneo hilo, Peter Shake aliwaomba wenyeji kuhama kutoka katika nyumba walizojenga kwenye makorongo kwa sababu zina hatarisha maisha yao.

"Tunaomba kwanza wananchi kwa unyenyekevu sana wale ambao mmejenga karibu na makorongo tafadhali mjaribu kutoka hapo na tuweze kuona tutasaidiana vipi kujenga nyumba mahali ambapo hatuwezi kupata hatari kama ambayo tumepata kwa siku hii," alisema Shake.

Maofisa wa kaunti ya Taita Taveta walmesema wanajaribu wawezavyo kuwapata waliotoweka ili kuipa familia yao amani

Baba mzazi wa Sabina, Rashid Mwamidi alikosa maneno baada ya kufahamishwa kuwa nyumba ya mwanawe imesombwa na mafuriko na alikumbuka mazungumzo yao ya mwisho kabla ya mafuriko kuisomba nyumba hiyo.

"Akaja hapa darajani akanipigia simu baba hata nyumba hakuna. Nyumba imeshasombwa," amesema.


Imeandaliwa na Pelagia Daniel