Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo 10 ya kipekee kuhusu Vatican

Muktasari:

  • Nchi ya Vatican inatajwa kuwa na sifa za kipekee kutokana na muundo wake wa uongozi unaoshabihiana na mamlaka ya Kanisa Katoliki duniani.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara katika nchi tatu ikiwamo Vatican.

 Mwananchi Digital imekuandalia makala maalumu kuhusu mambo ya kipekee yanayopatikana katika nchi hiyo ambayo pia ni makao makuu ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani.

Rais Samia atafanya ziara hiyo Februari 11 na 12, 2024, ikitanguliwa na atakayoifanya nchini Indonesia kati ya Januari 24 na 26, mwaka huu na baadaye Februari 13 na 14, 2024 nchini Norway.

Loading...

Loading...


1. Nchi ndogo zaidi duniani

Ikiwa na eneo la kilomita za mraba 0.44, kwa mujibu wa tovuti ya world population review, Vatican ina jumla ya watu 523 hadi mwaka 2024, hivyo kuifanya kuwa nchi ndogo zaidi duniani. Kutokana na udogo huo, tovuti ya Vatican history inasema nchi hiyo unaweza kumaliza kuitembelea ndani ya saa moja.


2. Yapakana na Jiji la Roma kwa kiasi kikubwa

Sifa nyingine ya kipekee ya nchi hiyo ni kupakana na Jiji la Roma lililopo Italia. Hata hivyo, licha ya kupakana na jiji hilo kwa kiwango kikubwa, bado Vatican ina mamlaka kamili na inatawaliwa na Papa (Askofu wa Roma) pia ni makao makuu ya Kanisa Katoliki.

Vatican ilitangazwa kuwa huru kutoka Italia Februari 11, 1929 kwa kutiwa saini Mkataba wa Lateran kati ya Papa Pius XI na Benito Mussolini aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia katika kipindi hicho.


3. Vatican haina gereza

Vatican huenda likawa Taifa pekee duniani ambalo halina gereza. Nchi hiyo ina mahabusu chache ambazo watuhumiwa huwekwa kizuizini kabla ya maamuzi ya kesi. Watakaopatikana na hatia hutumikia kifungo katika magereza ya Italia kulingana na Mkataba wa Lateran, gharama za kifungo zinalipwa na Serikali ya Vatican.


4. Makao makuu anayoishi Papa yalijengwa kwa miaka 120.

Basilica ya Mtakatifu Petro, ambayo pia ni makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani ilichukua miaka 120 kukamilika ujenzi wake.

“Ujenzi ulianza Aprili 18, 1506 na kukamilika Novemba 18, 1626. Ukubwa wake ni mita za mraba 23,000,” imeandikwa na tovuti ya kimataifa ya utalii ya ‘Get your guide’ kwa msaada wa makumbusho ya Taifa ya Vatican.


5. Papa analindwa na walinzi wa Uswisi

Japokuwa ni nchi yenye mamlaka kamili lakini kiongozi wake ambaye ni Papa analindwa na wanajeshi kutoka nchini Uswisi, kulingana na taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa Vatican history, idadi ya walinzi hao ni 135.

“Waliajiriwa kwa mara ya kwanza mwaka 1506 na Papa Julius II ambaye alihitaji ulinzi binafsi ili kujilinda na maadui wa Kanisa. Wanatambulika kwa urahisi katika sare zao zenye mchanganyiko wa rangi.

“Sifa za walinzi hao kutoka Uswisi ni lazima awe mwanamume kati ya miaka 19 na 30, mwenye urefu wa futi tano na inchi nane (5’ 8’’), lazima awe Mkristo na awe amemaliza mafunzo ya msingi ya kijeshi,” imeandika tovuti hiyo.


6. Hakuna uraia wa kuzaliwa Vatican

Kitu kingine cha tofauti katika nchi hiyo ni ngumu kuwa na raia wa kuzaliwa kwa sababu hakuna hospitali kwa ajili ya kujifungulia, hivyo unapewa uraia kwa misingi ya kuteuliwa kufanya kazi katika nafasi fulani katika huduma ya kiti kitakatifu.

“Uraia huo unatolewa kwa wanandoa, wazazi na jamaa wengine wanaoishi pamoja. Baada ya uteuzi kutenguliwa, uraia huvuliwa,” imeandika tovuti ya Vatican history.


7. ATM yenye lugha ya Kilatini

Vatican hutumia Kilatini kama lugha rasmi, hivyo hata ATM zake hutoa maelekezo kwa lugha hiyo, japokuwa bado Kiitaliano hutumika kama lugha rasmi katika masuala mengine.


8. Njia fupi ya reli duniani

Vatican pia inashikilia rekodi ya kuwa na njia ya reli fupi zaidi duniani, ambayo ina urefu wa mita 300, huku njia zikiwa mbili.

“Njia za reli na kituo cha treni zilijengwa wakati wa Papa Pius XI. Inatumika kwa usafirishaji wa bidhaa, hivyo hakuna treni ya abiria,” imeandika tovuti ya Vatican history.


9. Inamiliki darubini Arizona, Marekani

Vatican mwaka 1981 ilinunua darubini inayotumia teknolojia ya hali ya juu ambayo ni miongoni mwa darubini kubwa duniani.

“Inakaa juu ya Mlima Graham Kusini Mashariki mwa Arizona nchini Marekani. Vatican hufanya utafiti wa unajimu kutokea hapo,” imeandika tovuti ya Vatican history.


10. Miongoni mwa maeneo ya urithi wa dunia

Maeneo mbalimbali ya kihistoria hutambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) lakini kwa kipekee, shirika hilo limeitambua nchi yote ya Vatican kwa ujumla kuwa urithi wa dunia.

“Iliorodheshwa kuwa miongoni mwa urithi wa dunia mwaka 1984,” imeandika tovuti ya Vatican history.