Mashambulizi ya Iran yajeruhi binti Israel

Watu wakiangalia mabaki ya kombora lililotunguliwa huko Jordan. Picha na AFP

Muktasari:

Vipande vya makombora ya Iran yaliyotunguliwa vimeangukia kwenye nyumba na kusababisha binti wa miaka saba kujeruhiwa

Tel Aviv. Mashambulizi ya anga ya Iran dhidi ya Israel yamesababisha kujeruhiwa kwa binti mwenye umri wa miaka saba, kusini mwa Israel.
Usiku wa kuamkia leo Iran iliishambulia Israel kwa ndege zisizo na rubani zenye makombora takriban 300 na makombora yanayojiendesha yenyewe 120.
Hata hivyo, kwa msaada wa  majeshi ya Marekani makombora na ndege zisizo na rubani zilitunguliwa kabla ya kusababisha madhara, huku Uingereza na Ufaransa zikishiriki kulinda anga.
Kutunguliwa kwa makombora, vipande vyake ndivyo vimeelezwa kusababisha kujeruhiwa kwa binti huyo mwenye umri wa miaka saba aliyekuwa amelala nyumbani kwao.
Mohammed ambaye ni baba wa binti huyo aiambia ‘The Times of Israel’ kwamba, vipande vya makombora yaliyotunguliwa ndiyo viliangukia kwenye nyumba yao walimokuwa wamelala na kumjeruhi binti yake.
“Kilianguka kwenye nyumba yetu saa nane usiku. Binti alikuwa amelala na baada ya kuangukiwa na kipande hicho tumempeleka kwenye hospitali ya Soroka,” amesema.
Mohammed na familia yake wanaishi katika Mji wa Bedouin kusini mwa Israel.
Hata hivyo, hakuna taarifa zaidi za majeruhi au vifo kufuatia shambulio hilo la Iran.
Nchi zilizoshiriki kulinda Israel
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin amesema wanajeshi wa Marekani walishiriki kuyatungua makombora na ndege zisizo na rubani za Iran.
Ndege za kivita za Uingereza pia zilishiriki kuweka ulinzi, huku msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Israel amesema ndege za kivita  za Ufaransa zilishiriki kulinda anga ya Israel.
Serikali ya Jordan nayo imetoa taarifa ikisema imetungua makombora yaliyokuwa yakielekea kwenye anga lake.
Wakati anga la Israel limefunguliwa tena leo asubuhi baada ya kufungwa kwa muda, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, ameshutumu kitendo cha Iran cha kufanya mashambulizi hayo huku akisema dunia haiwezi kumudu vita vingine.
Taarifa ya Guterres imezitaka pande zote kuepuka mashambuzli zaidi kunakoweza kusababisha kuibuka vita kubwa eneo la Mashariki ya Kati.
(Imeandaliwa na Noor Shija)