Mbunge Uganda ajibu mapigo Spika kufutiwa viza
Muktasari:
- Mbunge huyo amefichua hayo alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusu sheria mpya ya kupinga mapenzi ya jinsi moja jana Mei 29, 2023 katika viwanja vya Bunge, ikiwa ni saa chache baada ya Rais Yoweri Museveni kutia saini muswada wa kupinga ushoga kuwa sheria.
Kampala. Mbunge wa Bugiri nchini Uganda, Asuman Basalirwa amewataka Wabunge na Waganda kwa ujumla, kutoyumbishwa na hatua zichuliwazo na nchi za magharibi baada ya Bunge la nchi hiyo kupitisha sheria mpya dhidi ya wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Basalirwa ambaye kimsingi ndiye mtoa hoja ya uliokuwa muswada na sasa ni sheria, ambapo mtu yeyote atakayekutwa hatiani, atakabiliwa na adhabu ya ama kifungo cha maisha au kunyongwa.
Mbunge huyo ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusu sheria hiyo mpya jana Mei 29, 2023 katika viwanja vya Bunge, ikiwa ni saa chache baada ya Rais Yoweri Museveni kutia saini muswada kuwa sheria.
Wito wa Basalirwa, unakuja baada ya kuwa amefichua taarifa za kufutiwa viza ya Marekani kwa Kiongozi wa Bunge la Uganda, Spika Anita Among, na kwamba maamuzi yaliyofanyika ni ya Waganda na ni azimio la Waganda.
"Tumepata taarifa kuwa ubalozi wa Marekani nchini Uganda, umemfutia Spika wa Bunge Anita Among viza yake…lakini hili ni azimio la Waganda, tunapashwa kushikilia msimamo kwani ni hatua kuu iliyofikiwa na hatupashwi kudoofishwa,” amesema na kuongeza;
“...Nadhani walitafuta kujua kama nina viza ya Marekani na hawakupata, kwa hiyo, mwathirika wa kwanza ni Spika. Ninaelewa Serikali ya Uingereza nayo iko mbioni kufanya hivyo. Kwanza hatuna tatizo na namna nchi hiyo inavyosimamia mambo yake,” amesema na kuongeza;
“Ikiwa kwa hekima na demokrasia yao hawatutaki katika nchi zao, hiyo ni haki yao na isitokee mtu yeyote kuilaumu Marekani au Uingereza kwa kitendo chao cha kufuta viza. Sitalalamika, wala kuchukia ubalozi wowote kwa kufuta visa ya mtu yeyote.”
Hata hivyo, alisema kuwa tatizo lake ni zuio hilo ambalo anadai linawalenga watu wachache na kuwaacha wahusika wengine wengine muhimu.
Mfano amesema: “Sheria hii ilitiwa saini na Rais wa Uganda, sasa naomba niwaalike Marekani, Canada, Uingereza, Umoja wa Ulaya (EU) pia kufuta viza za Rais Yoweri Museveni," amesema na kuongeza;
"Naomba pia niwaalike kufuta viza vya wabunge wote isipokuwa wawili. lakini pia kuwe na marufuku ya kusafiri siyo tu kwa Basalirwa na Anita Among, wote watuzuiwe,” amehoji.
Kwa mtazamo wa Mbunge huyo, anadhani ni vyema Waganda wote wakanyimwa viza za Marekani, Canada na Umoja wa Ulaya.
“....Kwa sababu huu umekuwa muswada wenye pande mbili zaidi katika historia ya nchi hii. Kwa hivyo, kwa nini umchague Basalirwa, Spika Anita Among. Hii inashanga! Hapana, ilitarajiwa. Binafsi nilizungumza na Bahati, aliniambia kwamba baada muswada kupita, ilikuwa ni changamoto kupata malazi katika hoteli za Marekani,” amefafanua.
Hata hivyo, bado haijafahamika iwapo hatua ya ubalozi huo ilihusiana na jukumu la Spika huyo kama kiongozi wa mhimiri huo ambao ulisimamia kuandaliwa kwa muswada, majadiliano na hata kupitishwa kwake na baadaye kusainiwa na Rais ambapo sasa sheria rasmi.
Haya yanatokea huku kukiwa na hofu kwamba wafadhili, hasa kutoka nchi za Magharibi wanaweza kupunguza michango yao ya fedha kufuatia kutungwa kwa sheria hiyo inayotoa adhabu ya hadi kifo kwa mtu atakayekutwa na hatia ya kujihusisha na makosa hayo.
Kwa mantiki hiyo, Basalirwa ameshauri: "Hebu tufikirie kutafuta washirika wa maendeleo sehemu zengine, niko tayari kupigania harakati za kwenda katika ulimwengu wa Kiarabu kutafuta msaada wa wafadhili. Tutaenda Saudi Arabia, Kuwait, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na nakisi hii ambayo inategemea kupungua, itajazwa na wahisani wapya kwa urahisi."
Mbunge huyo ameongeza kusema: “Kwa hivyo, tushirikiane tena, ikiwa hatujafikiria kuhusu Mashariki ya Kati na hasa ulimwengu wa Kiarabu ambako wanaheshimu maadili na maadili, basi twende huko.”
Kwa mujibu wa barua iliyoonwa na New Vision inaonyesha kuwa Ubalozi wa Marekani mjini Kampala ulimwandikia Among Mei 16, 2023 kumjulisha uamuzi huo.
“Serikali ya Marekani imebatilisha viza zako kutokana na taarifa ambazo zilikuja kupatikana baada ya utoaji wa viza hiyo. Hadi tarehe 12 Mei 2023; huna viza halali ya kusafiri hadi Marekani ingawa unakaribishwa kutuma ombi tena,” inaeleza sehemu ya barua hiyo, na kuongeza;
“Tafadhali tuma pasipoti yako kwa ubalozi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ili tuweze kufanya marekebisho yanayohitajika kwa viza yako.”
Hata hivyo alipofuatwa Msemaji wa Bunge Chris Obore amesema: “Nimesikia haya kutoka kwa watu ambao walikuwa kwenye mkutano na waandishi wa habari. Unajua mawasiliano ya kidiplomasia ni maalumu, yanaelekezwa kwa Spika moja kwa moja.”
Msemaji huyo wa Bunge la Uganda amefafamnua kuwa: "Siwezi kuthibitisha au kukataa kwamba ni kuhusu Muswada wa Kupinga Mapenzi ya Jinsi Moja. Ni Ubalozi wa Marekani pekee ambao unaweza kutoa muktadha unaofaa. lakini pia unaweza kujua kupitia Wizara ya Mambo ya Nje maana ndiyo chombo kinachoongoza katika mahusiano ya kidiplomasia.”
Na kwa upande wa Joseph Sabiiti ambaye ni Msaidizi wa Binafsi wa Spika Among, amesema: “Hakuna sababu iliyotolewa ya kufutwa viza. Kwa hivyo, hatuwezi kuthibitisha ikiwa ubatilishaji wa viza una uhusiano wowote na muswada uliopitishwa kuwa sheria."
Hata hivyo, mtandao wa New Vision umemnukuu Mshauri wa Masuala ya Umma kwenye ubalozi huo mjini hapa Ellen Masi akisema: “Rekodi za visa ni siri chini ya sheria za Marekani; kwa hiyo, hatuwezi kujadili maelezo ya kesi hii binafsi."