Mchungaji Mackenzie aibua mpya akiomba kununuliwa chakula

Muktasari:

  • Mhubiri Paul Mackenzi kutoka Kenya ambaye amevuma siku za karibuni, amewashangaza watu baada ya kuwataka waandishi wa habari waliofika mahakamani kumnunulia maziwa na mkate kwa kupitia hela walizopata katika kesi inayomkabili akidai kuumwa na njaa.

Kenya. Mchungaji Paul Mackenzi wa nchini Kenya amewashangaza watu mahakamani baada ya kuwataka waandishi wa habari kumnunulia maziwa na mkate kwa fedha wanazozipata kupitia habari za kesi yake.

Mackenzie leo Jumatatu Juni 5, 2023 amewaomba wanahabari waliofika mahakamani hapo kununulia chakula hicho kwasababu alikuwa na njaa.

"Fedha mliyopata hamuwezi kuninunulia hata mkate? mimi nimezuiwa siwezi kupata fedha. Si muende mniletee angalau pakiti ya maziwa," Mackenzie amewaambia wanahabari.

Mhubiri huyo ambaye anadaiwa kumiliki msitu wa Shakahola ameendelea kusisitiza kwamba hana makosa na kuwa amezuiliwa kinyume cha sheria.

Mackenzie ameendea kukaa rumande baada ya upande wa mashtaka kuiomba mahakama kuwaongezea muda zaidi ili wakamilishe uchunguzi wa vifo vinavyoripotiwa kutoka katika msitu wa Shakahola ulioko katika kaunti ya Kilifi.

Waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki amenukuliwa akisema kuwa Serikali haitaruhusu Mackenzi kuachiliwa.

Mackenzie aliyeko kizuizini, anachunguzwa kwa kuwashawishi waumini wa kanisa lake la Good News International kufa kwa njaa kwa ahadi ya kukutana na Yesu.