Mchungaji Odero aachiwa kwa dhamana
Muktasari:
- Hakimu Mwandamizi Mahakama ya Shanzu Joe Omido, amemwachilia mhubiri huyo kwa bondi ya Sh3 milioni au dhamana ya Sh1.5 milioni pesa taslimu fedha za kenya.
Kenya. Mahakama nchini Kenya imemwachilia mchungaji Ezekiel Odero kutoka mikononi mwa polisi, huku ikitanabaisha kuwa sababu zilizotolewa na jeshi hilo ili liendelee kumshikilia zaidi, hazina mashiko.
Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya Shanzu Joe Omido, amemwachilia mhubiri huyo kwa bondi ya Sh3 milioni au dhamana ya Sh1.5 milioni pesa taslimu fedha za kenya.
Mchungaji Odero ametakiwa kuripoti polisi mara moja kwa wiki na amezuiwa kutoa maoni yake kuhusu mauaji ya Shakahola.
Masharti ya kuachiliwa kwake yataendelea hadi uchunguzi utakapokamilika au pale atakaposhtakiwa rasmi mahakamani.
Odero na mwinjilisti mwenzake wa televisheni Paul Mackenzie wanachunguzwa kuhusiana na sakata la Shakaloha, kaunti ya Kilifi, ambako kumeshuhudiwa mauaji ya zaidi ya watu mia moja, waliofariki kutokana na njaa, chini ya maagizo ya Mackenzie.
Mambo ambayo mhubiri Odero anachunguzwa kwayo, ni pamoja na mauaji, kusaidia kujitoa mhanga, utekaji nyara, itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya ubinadamu, ukatili wa watoto, ulaghai, utakatishaji fedha na kuwa chanzo cha uhalifu.
Serikali ilitaka kumweka kizuizini mwinjilisti huyo wa televisheni kwa siku 30 zaidi huku uchunguzi ukiendelea.
Waendesha mashtaka waliambia mahakama ya Mombasa kwamba wana taarifa mpya kuhusu vifo vya watu wa madhehebu ya Shakahola, ambayo inadaiwa kuwa kasisi Mackenzie anachunguzwa.
Mwendesha mashtaka alisema uchunguzi wa maiti kwenye baadhi ya miili iliyofukuliwa huko Shakahola unaonyesha kuwa baadhi ya waathirika, wengi wao wakiwa watoto, walikufa kutokana na kunyongwa. Serikali iliita hii "habari mpya."
Serikali pia ilikiri kwamba vifo vilivyotokea katika kanisa la Odero viliripotiwa kwa polisi, lakini ikaeleza kuwa wakati wa ripoti hii, hakukuwa na sababu ya kushuku kisa cha uhalifu.
Mchungaji huyo kupitia kwa mawakili wake, awali alikiri kuwa watu 15 wamefariki dunia walipokuwa wakitafuta msaada wa kiroho katika Kituo cha Maombi ya Maisha Mapya na Kanisa lake, katika kipindi cha mwaka mmoja na mwezi mmoja kilipoanza kazi.
Kupitia kwa mawakili wake Cliff Ombeta, Danstan Omari na Shadrack Wamboi, Odero amesema 15 hao walitafuta usaidizi wake wakiwa katika hali mbaya.