Mackenzie na sakata la vifo vya waumini Kenya

Bango la mkutano wa injili wa mchungaji Ezekiel Odero jijini Dodoma, mkutano huo ulipangwa kufanyika Aprili 28 hadi 30 mwaka huu

Dar es Salaam. Wakati kiongozi wa dhehebu tata la Kikristo Kenya, Mchungaji Paul Mackenzie akitarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo, Mwinjilisti maarufu wa Televisheni nchini humo, Ezekiel Odero amekamatwa wakati akijiandaa kufanya mkutano wake wa injili jijini Dodoma.
Ezekiel, aliyetarajiwa kuhubiri injili nchini hapa, polisi wa Kenya wanaendelea kuchunguza uhusiano wake na Mchungaji Mackenzie kwa madai kuwa, vifo zaidi ya 100 vilitokea karibu na eneo la kanisa lake.
Jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno alikiri kuufahamu mkutano huo, akisema walikuwa wamefuata taratibu zote za kuandaa mikusanyiko.
“Ukiangalia Dodoma yote utakuta kuna mabango yamewekwa kuna mchungaji kutoka Kenya atakuja Dodoma, kwa hiyo na sisi taarifa tulikuwa tunayo, hakuna mtu atakayezuiliwa kufanya mkutano wa Injili au aina nyingine akakataliwa ikiwa atafuata sheria za nchi,” alisema Otieno.
Mkutano huo ulipaswa kuanza Aprili 28 hadi 30, 2023 katika viwanja maarufu vya Wachina ambako hata hivyo jana eneo hilo lilionekana kimya bila maandalizi wala shamrashamra zozote.
Alisema kuna utaratibu wa kuandika barua ya maombi kwa Jeshi la Polisi kuhusu mkusanyiko, huku akisisitiza ikiwa mkutano huo utahitajika kufanywa tena, wahusika watatakiwa kutoa taarifa upya.
Aksa Ndalu, ambaye hujihusisha na timu ya maombi makanisani alisema hamasa ilikuwa kubwa kuhusu mkutano huo, ingawa hajui lilipo Kanisa la New Life lililoandaa mkutano.
Ndalu alisema mkutano huo ulikuwa na hamasa kubwa, lakini timu ya maombi haikuwa na taarifa kama wanavyofanya wengine.
Katika eneo la Kikuyu lililoelekezwa kuwa kanisa hilo lipo, Mwananchi ilifika na kanisa lililopo si New Life.
Namba za simu zilizoandikwa kwenye bango la tangazo la mkutano hazikupatikana zote, licha ya moja kuandikwa kwa namba za Tanzania na nyingine namba za nje ya nchi.

Kuhusu Mchungaji Mackenzie

Mbali na Odero kuhusishwa na mauaji, waumini wa Mchungaji Mackenzie waliokufa kwa njaa baada ya kuamriwa na kasisi huyo wafunge, wafe ili wakakutane na Yesu, zaidi ya 100 wamekufa hadi sasa.
Wakati shughuli za ufukuaji miili kwenye makaburi ya pamoja ikiendelea katika ardhi yake Kenya, Mchungaji Mackenzie ambaye ni mwanzilishi wa Kanisa la The Good News International Ministries (GNIM), anadai alilifunga kanisa hilo miaka minne iliyopita baada ya kuhudumu kwa takriban miongo miwili.
Hata hivyo, wakati akidai hayo, bado kuna mahubiri yake yanayopatikana mtandaoni baadhi yakionekana kurekodiwa baada ya kulifunga kanisa hilo.
Katika video moja ya mtandaoni, kwa sauti ya shauku Mchungaji Mackenzie anatoa mahubiri yake mbele ya mkusanyiko mkubwa wa watu kwa msisimko wa mada zake zenye itikadi kali.
Bango katika moja ya video zake za mtandaoni linasomeka: “Tunakaribia kushinda vita ... Mtu yeyote asirudi nyuma ... safari inakaribia kufika mwisho.”
Mojawapo ya video kwenye chaneli ya YouTube ya kanisa lake inasema hivi: “End Time Kids” na inaonyesha vikundi vya watoto wadogo wakizungumza mbele ya kamera.
Ingawa haijulikani ni lini mahubiri hayo yalirekodiwa, ipo moja inayorejea tukio lililofanyika jijini Nairobi Januari 2020 inayokinzana na madai ya Mchungaji Mackenzie kuwa alilifunga kanisa hilo miaka minne iliyopita, kwa maana ya mwaka 2019.
Kwa mara kadhaa, mwaka 2017 na baadaye mwaka 2018, alikamatwa kwa kuhimiza watoto wasiende shule akidai elimu haitambuliwi katika Biblia.
Mchungaji Mackenzie amelaani elimu kwa kuendeleza mapenzi ya jinsia moja kupitia programu za elimu ya ngono.
Alikaririwa na gazeti ‘The Nation’ la Kenya akisema: “Niliwaambia watu elimu ni mbaya ... watoto wanafundishwa mapenzi ya jinsia moja.”
Inadaiwa pia alichukia tiba za kitabibu na aliwahimiza kina mama kuepuka kupata matibabu wakati wa kujifungua na waepuke kuwachanja watoto wao.
Katika mojawapo ya video hizo, mwanamke mmoja anasimulia jinsi alivyomsaidia mwingine kujifungua mtoto kwa njia ya maombi na bila haja ya upasuaji, akiongeza baadaye alipata “upako” wa Roho Mtakatifu na kumwonya jirani yake kutomchanja mtoto wake.
Kisha mchungaji anaunga mkono maoni yake akisema chanjo si lazima huku akidai madaktari humtumikia Mungu tofauti.” Pia, aliwahimiza wanawake kutosuka nywele zao au kuvaa mawigi na mapambo mengine.

Alama za shetani

Sehemu kubwa ya mahubiri ya mchungaji huyo yanahusu ‘kutimia kwa unabii wa Biblia’, hasa siku ya hukumu. Hata maudhui ya mtandaoni ya kanisa hilo yamejikita sana kwenye machapisho yanayohusu mwisho wa dunia, maangamizi yanayokaribia na hatari zinazodhaniwa kuwa za sayansi.
Sehemu nyingine ya maudhui hayo ni onyo analotoa mara kwa mara kuhusu nguvu za kishetani zilizo na uwezo unaosemekana umejipenyeza kwenye ngazi za juu zaidi za mamlaka duniani kote.
Katika video hizo amezungumza sana habari ya kile anachokiita ‘New World Order’, nadharia inayohusu njama za wasomi wa kimataifa kuleta Serikali ya kimabavu ya ulimwengu na kuchukua nafasi ya mataifa.
Anadai kuwa Kanisa Katoliki, Umoja wa Mataifa na Marekani wako nyuma ya nguvu hizo na kwamba wao ni wakala wa shetani.
Lakini mahubiri yote hayo yaliendelea na kufikia hatua ya kusababisha vifo vya waumini zaidi ya 100 waliogunduliwa wakiwa wamezikwa kwenye makaburi ya halaiki katika Msitu wa Shakahola karibu na Mji wa Pwani wa Malindi.
Tukio hilo limewashtua Wakenya na walimwengu wengine, huku kukiwa na hofu maiti zaidi zinaweza kupatikana wakati wakiendelea kufukua makaburi.
Wapelelezi wanasema waathirika wengi ni watoto katika kile kilichopewa jina la ‘Mauaji ya Msitu wa Shakahola.’
Hayo yametendeka katika kanisa linalojulikana kama The Good News International linalojulikana sana kama dhehebu la Malindi (na hapo awali kama Kanisa la Mtumishi PN Mackenzie).

Mwanzo wa Kanisa la Mackenzie

Kanisa hilo lililoko Shakahola, Magarini katika Kaunti ndogo ya Kilifi Kenya lilianzishwa mwaka 2003 na Paul Mackenzie akishirikiana na mkewe, Joyce Mwikamba.
Kabla ya kuanzisha kanisa hilo, Mackenzie alifanya kazi kama dereva teksi jijini Nairobi tangu 1997 hadi 2003. Baada ya kanisa kuanzishwa mwaka 2003, alishtakiwa mara nne kutokana na mahubiri yake, lakini aliachiwa kwa sababu ya kukosekana ushahidi.
Kanisa lilipoanza kupata mafanikio kwa maana ya kuongezeka kwa waumini, Mackenzie na Mwikamba walihamia Kijiji cha Migingo kilichoko Malindi.
Mackenzie alifanikiwa kukusanya wafuasi wengi na kuwaaminisha alikuwa anawasiliana na Mungu moja kwa moja.
Mwaka 2016, mmoja wa wafuasi wa kanisa hilo aliuza mali zake katika Kisiwa cha Lamu na kumpatia Mackenzie KSh20 milioni (Sh350 milioni).
Mhubiri huyo anadaiwa kutumia pesa hizo kununua mali katika miji ya Mombasa na Malindi, magari mawili na kufadhili kituo cha televisheni kutangaza mahubiri yake.
Hata hivyo, Bodi ya Filamu ya Kenya ilikifungia kituo chake cha TV 2018.
Hatua ya mfuasi huyo iliwashawishi wafuasi wengine kadhaa kufuata mfano huo, wakiuza mali zao na kupeleka fedha hizo kanisani kwa Mackenzie.
Mwaka 2017, Mackenzie na Mwikamba walishtakiwa kwa kuendeleza itikadi kali ya kidini, ikiwa ni pamoja na kuwanyima watoto huduma ya afya na elimu na kuendesha shule na televisheni isiyo na leseni wala isiyoidhinishwa na Serikali.
Lakini watoto kadhaa walikufa kwa kukosa huduma za afya na mwaka 2017, Serikali iliwaokoa watoto 93 katika kanisa lake.
Mwaka 2018 alituhumiwa na baadhi ya wananchi, wanaharakati na Mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa kwa kuwashawishi watoto kuacha shule bila idhini ya wazazi.
Kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa madai hayo, waliachiwa huru.
Mwaka 2019, Mackenzie alikamatwa kwa kuushawishi umma kususia usajili wa Huduma Namba Kenya na kuifananisha huduma hiyo na ‘Alama ya Mnyama.’
Alishtakiwa kwa kosa la kuwatia watu kasumba mbaya na kuwateka nyara watoto ili washiriki ibada zake.
Hapo napo aliachiwa huru kwa kukosekana ushahidi dhidi yake.
Ilikuwa baada ya tukio hili ndipo alifunga kanisa lake huko Migingo na kuhamia wilaya ya mbali huko Shakahola.

Kupatikana kwa miili

Aprili 25 mwaka huu, maiti 89 zilipatikana katika Msitu wa Shakahola, karibu na Malindi, Kenya.
Manusura waliookolewa walisema Mackenzie aliwaamuru kujiua kwa njaa ili wakakutane na Yesu.
Ingawa miili mingi imepatikana, zaidi ya watu 200 wanaripotiwa kutoweka au kutojulikana waliko.
Kwa mujibu wa tovuti ya kanisa hilo pamoja na taarifa mbalimbali za vyombo vya habari, Mackenzie na wenzake wanadaiwa kuwa ni wafuasi wa wenye ‘Imani ya Nyakati za Mwisho’ iliyoanzishwa na Kasisi William Marrion Branham.
Kasisi huyo ana mtandao wa kimataifa usio rasmi wa makanisa yaliyoibuka. Wapelelezi wa Kenya walikuta vijitabu vya mafundisho ya Branham katika wilaya hiyo ambavyo waandishi wa habari walionyeshwa.
Kasisi William Branham aliyezaliwa Aprili 1909 na kuaga dunia Desemba 1965 alikuwa mhudumu wa Kikristo wa Marekani na ‘mponyaji wa imani’ ambaye baada ya Vita Kuu II alianzisha kile alichokiita ‘uamsho wa uponyaji’ akijiita nabii wa upako wa Eliya wa Biblia.
Alidai yeye ndiye alikuja kuandaa ujio wa pili wa Yesu Kristo; baadhi ya wafuasi wake wamekuwa wakijulikana kama watu wa ibada ya “siku ya mwisho ya hukumu.”
Mafundisho ya Mackenzie yameelezwa kuwa yanasisitiza sana maonyo ya siku ya mwisho au ‘kuja kwa Yesu mara ya pili.’
Mackenzie anapingana na “maovu ya maisha ya kimagharibi” ambayo ni pamoja na huduma za matibabu, elimu, chakula, michezo, muziki na ubatilifu wa maisha.”
Katika wimbo ulioitwa ‘The Antichrist’ (Mpinga Kristo) katika chaneli yake ya YouTube analishutumu Kanisa Katoliki, Marekani na Umoja wa Mataifa kama mawakala wa shetani.
Mackenzie anaamini mfumo wa Vitambulisho vya Taifa wa Kenya wa ‘kibayometriki’ unaoitwa ‘Huduma Namba’ ni ‘Alama ya Mnyama’ kulingana na mafundisho ya Branham.
Alikuwa akiwasisitiza wafuasi wake siku ya mwisho iko karibu.
Wakati wafuasi wengi wa kundi hilo ni Wakenya, baadhi wanatokea Tanzania, Uganda na Nigeria, kwa mujibu wa jarida la mtandaoni la ‘The Tablet.’

Polisi waanza kulichunguza kanisa

Mapema Aprili mwaka huu, mwanamume mmoja alitoa taarifa polisi baada ya mkewe na binti yake kuondoka Nairobi na kujiunga na Mackenzie katika Kaunti ya Kilifi na hawakurejea tena nyumbani.
Polisi walipoanza kufanya uchunguzi wa tukio hilo katika kanisa hilo waliwakuta watu waliodhoofika na makaburi.
Wafuasi kadhaa wa kundi hilo waliokolewa na polisi. Walipohojiwa walisema waliamriwa wafe kwa njaa ili “wakakutane na Yesu.”
Waumini 15 walikuwa katika hali mbaya sana na walikimbizwa hospitali, wanne miongoni mwao walifariki dunia hata kabla ya kufika hospitalini.
Kwa wiki tatu zilizofuata, polisi walipekua eneo la ekari 800 (kilomita 3.2) na kukuta makaburi zaidi yaliyochimwa kwa kina kifupi.
Kulikuwa pia na manusura wa ziada waliokuwa wakifa kwa njaa kadiri muda ulivyosogea.
Miili mingi ya mwanzo kupatikana kutoka makaburini ilikuwa ya watoto. Polisi wa Kenya wanaamini katika kaburi moja kulikuwa na miili ya watu watano wa familia moja, watoto watatu na wazazi wao.
Kuna makaburi mengine yalikuwa na miili hadi sita ndani yake, baadhi ya miili haikuzikwa.
Polisi pia, waligundua idadi ya watu wengine waliodhoofika, akiwamo mmoja aliyekuwa amezikwa akiwa hai siku tatu zilizokuwa zimepita, baadaye kupelekwa hospitali kwa matibabu.
Mamlaka za Serikali za eneo hilo ziliomba msaada kutoka mamlaka nyingine ili kuongeza juhudi za uokozi.
Serikali inaamini idadi isiyojulikana ya watu waliotoweka watakuwa bado wamejificha msituni kuukwepa mkono wa Dola huku wakiendelea kufunga.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliohojiwa na polisi, Mackenzie aliwaambia wafuasi wake, “mfungo utahesabiwa tu ikiwa watakusanyika pamoja na kuwapa shamba lake kama mahali pa kufungia. Hawakupaswa kuchanganyika na mtu yeyote kutoka ulimwengu wa ‘nje’ ikiwa wanataka kwenda mbinguni na walitakiwa kuharibu nyaraka zote zilizotolewa na Serikali, vikiwamo Vitambulisho vya Taifa na vyeti vya kuzaliwa.”

Kufukuliwa miili

Kufikia Aprili 26, vifo 103 vilikuwa vimeripotiwa ikiwa ni pamoja na wanane waliookolewa lakini wakafariki baadaye.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya liliripoti watu 311, wakiwamo watoto 150, wamepotea. Kufikia Aprili 24 manusura 39 waliodhoofika walikuwa wameokolewa.
Mackenzie na washiriki wengine 14 wa kanisa hilo walikamatwa na wako chini ya ulinzi wa polisi.
Aprili 25 timu za upekuzi zililazimika kusitisha ufukuaji wa miili hadi 90 ya kwanza ifanyiwe uchunguzi kwa sababu chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi kilizidiwa kwa kukosa nafasi ya kuihifadhi miili hiyo.
Baada ya upelelezi wao, wapelelezi kutoka kitengo cha mauaji Kenya walisema Mackenzie aliwachanganya waumini wake kwa kutumia Theolojia ya Siku za Mwisho ya William Branham na kuwafanya wasadiki njaa inaweza kuwaharakisha kuyatoroka maisha haya ili wakutane na Yesu.”
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Rais wa Kenya William Ruto alisema, “Mafundisho ya Mackenzie yalikuwa kinyume na dini yoyote halisi.”
Sasa Mackenzie yuko mikononi mwa polisi akisubiri kesi yake kuanza.

Mchungaji Ezekiel

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi nchini Kenya wamemkamata mwinjilisti maarufu wa Televisheni, Ezekiel Odero kufuatia mauaji ya watu hao, huku pia wakichunguza uhusiano wake na Mchungaji Mackenzie.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Ezekiel alikamatwa baada ya polisi kukagua eneo lililokuwa na mazishi karibu na kanisa lake.
“Asubuhi hii tumemkamata Mchungaji Ezekiel Odero kwa madai ya vifo vilitokea katika eneo lake,” alisema Kamishna wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Rhoda Onyancha.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kithure Kindiki alisema Polisi waliopoa miili zaidi ya 100 ya waliokuwa wamezikwa katika kanisa hilo.
Mchungaji huyo hakujibu lolote kuhusu madai hayo na anatakiwa kufikishwa mahakamani Ijumaa ijayo.

Nyongeza na Mainda Mhando, Hàbel Chidawali (Dodoma)