Mfahamu Judith Suminwa, mwanamke wa kwanza kuwa Waziri Mkuu DRC

Waziri Mkuu mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Judith Suminwa.

Muktasari:

Judith Suminwa anakuwa mwanamke wa kwanza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwa Waziri Mkuu akichukua nafasi ya Jean-Michel Sama Lukonde aliyejiuzulu wiki mbili zilizopita

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza katika historia yake, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imempata Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke, Judith Suminwa.

Tuluka aliteuliwa na Rais Felix Tshisekedi Aprili mosi, mwaka huu, akichukua nafasi ya Jean-Michel Sama Lukonde aliyejiuzulu wadhifa huo Februari mwaka huu.

Kuapishwa kwa Tshisekedi kwa muhula wa pili Januari mwaka huu kulianzisha jitihada kubwa za kupata muungano wa walio wengi katika Bunge la Taifa, jambo ambalo ni sharti muhimu kabla ya kumteua Waziri Mkuu na kuunda Serikali.

Suminwa anatarajiwa kutangaza Baraza jipya la mawaziri siku chache zijazo. Waziri mkuu anaongoza Serikali ambayo pia inaundwa na mawaziri na manaibu waziri.

Waziri Mkuu mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Judith Suminwa.

Jukumu lake la kwanza ni kuunda Serikali mpya katika muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Rais Tshisekedi.

Kwa upande wa kiuchumi, matarajio ya Wacongo yameongezwa kutokana na kushuka kwa thamani kwa sarafu ya nchi hiyo.

Matatizo ya kiuchumi yamehusishwa na mzozo wa usalama mashariki mwa nchi hiyo na katika miji mikubwa, pamoja na Kinshasa, ambako ujambazi wa mijini unaleta changamoto kubwa kwa viongozi wa nchi.

Katika maneno yake ya kwanza, Waziri Mkuu mpya alitangaza: “Najua kwamba kazi ni kubwa na ina changamoto nyingi na kubwa, lakini kwa kuungwa mkono na Rais na umma, tutafika.”

“Mawazo yangu nayaelekeza mashariki na pembe zote za nchi yetu ambayo sasa inakabiliwa na migogoro na maadui ambao wakati mwingine wamejificha, hawajidhihirishi, lakini ambao watapatikana kwa njia moja au nyingine,” amesema Suminwa.

Waziri Mkuu huyo mpya hakuwa mwanasiasa mashuhuri nchini DRC hadi Machi 2023 alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mipango.

Ana shahada ya uzamili katika uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Libre de Bruxelles, Ubelgiji

Alifanya kazi katika sekta ya benki kabla ya kujiunga na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwamo Shirika la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP).

Suminwa ataongoza utawala mpya wa DRC baada ya ushindi wa Tshisekedi katika uchaguzi wa Desemba mwaka jana.

Licha ya kuongezeka kwa haraka wa uchumi wa DRC unaoendeshwa na sekta ya shaba, Taifa hilo linakabiliwa na migogoro inayoongezeka katika maeneo yake ya mashariki, pamoja na usimamizi wa utajiri mkubwa wa madini wa DRC.

Suminwa ni mwanasiasa wa DRC mwenye zaidi ya miaka 20 ya uzoefu wa kitaifa na kimataifa katika utawala wa kidemokrasia na amani jumuishi. Pia, ni mzoefu katika masuala ya fedha za umma kama vile ufuatiliaji wa masuala ya bajeti.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, alikuwa Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mipango. Uteuzi huo ulifanyika Machi 24, mwaka jana.

Pia, aliwahi kuwa Naibu Mratibu katika Baraza la Rais la Ufuatiliaji wa Mikakati (CPVS), na alisimamia ufuatiliaji wa kimkakati wa ahadi za Rais zilizoainishwa katika mpango wa Serikali.

Amekuwa pia ni mtaalamu wa Programu na Mratibu wa Nguzo ya Kuunganisha Amani na Demokrasia UNDP.

Kabla ya jukumu lake la UNDP, aliwahi kuwa mshauri mkuu katika Wizara ya Bajeti, na aliratibu Kitengo cha Usimamizi wa Mabadiliko, akisimamia utekelezaji wa mageuzi ya bajeti na utawala wa umma.

Safari yake kubwa ya kitaaluma ilianza UNDP mwaka 2002, na alishikilia nyadhifa mbalimbali za wataalamu wa programu kwa muongo mmoja, akiboresha ujuzi wake katika usimamizi wa miradi, utawala bora na utekelezaji wa mageuzi.