Kilichomchelewesha Rais congo kupata waziri mkuu
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi ametumia siku 115 tangu aingie madarakani kumpata waziri mkuu katika serikali yake mpya baada ya kukiondoa madarakani chama tawala cha Common Front for Congo (FCC) cha Joseph Kabila.
Machi mwaka huu FCC na CACH waliamua kuungana ili kuunda serikali ya umoja. FCC kina wabunge wengi ikilinganishwa na chama cha Rais Tshisekedi.
Licha ya ushindi kiongozi huyo amejikuta akichelewa kumpata waziri mkuu, pengine ilikuwa kumtafuta mtu mzoefu anayeweza kuinua uchumi.
Juzi Rais Tshisekedi alimteua Profesa Sylvestre Ilunga Ilunkamba kuwa waziri mkuu mpya wa DRC. Uteuzi huo umefanyika baada ya waziri mkuu aliyekuwepo Bruno Tshibala, kujiuzulu.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya uteuzi wake alisema kukuza uchumi ni kipaumbele cha serikali yake itakayoundwa baadaye.
‘‘Rais alinipokea na aliniambia kwamba kipaumbele cha serikali hii yetu ya muungano ni kuboresha maisha ya raia na kurejesha usalama,’’ alisema Illunga.
Raia wa Congo walikua wamesubiri zaidi ya miezi mitatu, bila ya kuwa na waziri mkuu mpya.
Kuhusu ni lini serikali itaundwa amesema kwa sasa mashauriano yanaendelea kati ya vyama vyao na kwamba mashauriano hayo yatakapokamilika serikali itatangazwa.
Slyvestre Illunga ambaye ni mwanasiasa mkongwe wakati wa utawala wa Rais Mobutu Seseko alikuwa naibu waziri wa uchumi, viwanda na biashara ya nje (1981-1983), naibu waziri wa mipango (1983-1984), naibu waziri asiye na wizara maalumu (1984-1986).
Pia, alikuwa mshauri mwandamizi wa Rais Mobutu wa masuala ya uchumi na fedha (1986-1987), naibu waziri wa mipango (1987-1990) na waziri wa fedha (1990-1991).
Kutokana na uzoefu wake katika masuala ya uongozi baadhi ya raia wana matumaini kuwa waziri mkuu huyo mpya ataleta mabadiliko hususan katika kupambana na rushwa ambayo imetajwa kuwa tatizo linalorudisha nyuma taifa hilo la maziwa makuu.
Mwanasiasa huyu mwenye umri wa miaka 78 ambaye pia ni miongoni mwa viongozi wa chama cha Joseph Kabila, alikuwa mkurugenzi wa kampuni ya reli ya Congo.
Tangu mwaka 2014 waziri mkuu huyu mpya alikuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni ya reli na wafanyi kazi wengi wa kampuni hiyo wamefanya kazi kwa muda mrefu bila kulipwa mishahara yao.
Kwa mujibu wa vyama vilivyomuunga mkono Joseph Kabila kulingana na jinsi walivyo na idadi kubwa ya waakilishi katika bunge la kitaifa, lile la seneti na majimboni wana haki ya kupewa asilimia 80 ya wizara huku wakidai chama cha rais mpya kinafaa kupewa asilimia 20.
Siku 100 za Tshisekedi
Rais Tshisekedi alianza kwa kutekeleza ahadi mbalimbali alizoziahidi ndani ya siku 100 za mwanzo. Moja ya ahadi hizo ni kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa ambao wengi wao walifungwa wakati wa utawala wa miaka 18 wa Kabila.
Rais huyo amewaachia mamia ya wafungwa hao ambapo kati yao wamo wanasiasa maarufu nchini humo, kama vile Frank Diongo, Diomi Ndongala na Firmin Yangambi ambao walishtakiwa kwa makosa ya usalama wa Taifa.
Ahadi nyingine alizoahidi Tshisekedi ni pamoja na kupambana na rushwa na kufungua uwanja wa kisiasa kwa vyama vya upinzani, ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikikandamizwa na serikali.
“Nitafanya kazi kwa bidii kuhakikisha kwamba tunatengeneza mazingira ambayo yatawawezesha Wacongo wote wanaoishi nje ya nchi kwa sababu za kisiasa wanarejea nyumbani haraka na kuendelea na shughuli zao kwa mujibu wa sheria,” aliahidi Tshisekedi Machi mwaka huu.