Milioni 110 wakimbia makazi yao mwaka 2023

Muktasari:

  • Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, limesema watu milioni 110, wamekimbia makazi yao, chanzo ikiwa ni vita vya Ukraine na Sudan, pamoja na mzozo wa Afghanistan, vimelazimisha mamilioni ya watu hao kutafuta usalama.

Geneva. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema idadi ya watu waliokimbia makazi yao duniani imefikia milioni 110, huku vita vya Ukraine na Sudan vikilazimisha mamilioni ya watu kutoka makwao.

Kwa mujibu wa kituo cha habari ‘Aljazeera’ hadi mwishoni mwa mwaka jana watu milioni 108.4 walikimbia katika maeneo yao kutokana na changamoto tofauti tofauti.

Idadi hiyo imeongezeka mwaka huu ambapo imefikia watu milioni 110, hasa kutokana na mzozo wa wiki nane wa Sudan, hayo yalielezwa na Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakimbizi Filippo Grandi.

Idadi ya jumla inajumuisha watu wanaotafuta usalama ndani ya nchi zao na pia wale ambao wamevuka mipaka. Wakimbizi na wanaotafuta hifadhi walifikia takriban asilimia 37.5 ya jumla hiyo.

Grandi amesema kabla ya mgogoro wa Syria mwaka 2011, kulikuwa na wakimbizi wapatao milioni 40 kulingana na shirika hilo. Lakini idadi hiyo imeongezeka kila mwaka tangu wakati huo.

Grandi amesema sababu za kawaida zinazowapelekea watu wengi kuhamishwa ni migogoro, mateso, ubaguzi, vurugu na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kati ya wakimbizi wote na wale wanaohitaji ulinzi wa kimataifa, karibu nusu yao walitoka nchi tatu tu Syria, Ukraine na Afghanistan, ripoti hiyo ilisema.

Mwishoni mwa 2022, Waukraine milioni 11.6 walisalia bila makazi pamoja na milioni 5.9 ndani ya nchi yao na milioni 5.7 nje ya nchi.

Hata hivyo, Grandi ameibua mjadala wa wasiwasi kuhusu nchi zinazoanzisha sheria kali zaidi za kuwapokea wakimbizi na kuwabana, bila kutaja nchi husika.

Nchi za mashariki mwa Umoja wa Ulaya, kama vile Poland na Hungary, zimekataa kuchukua mtu yeyote kutoka Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini yenye Waislamu wengi.