Mke adaiwa kumuua mumewe kwa fimbo

Muktasari:
- “Ukweli ni kwamba katika siku hiyo majira ya saa kumi na mbili asubuhi, marehemu alijeruhiwa vibaya upande wa kushoto wa kichwa na kusababisha kutokwa na damu nyingi baada ya kudaiwa kupigwa na fimbo na mkewe.”
Zambia. Polisi wilayani Nakonde, Mkoa wa Muchinga, Kaskazini mwa Zambia, wanamshikilia Astridah Namukonda, (19) kwa madai ya mauaji ya mume wake (26).
Kwa mujibu wa tovuti ya Diamond Tv ya nchini humo, tukio hilo limetokea Jumamosi Septemba 30, 2023 asubuhi baada ya kuzuka ugomvi baina ya wanandoa
Inaelezwa Astridah alimvamia mume wake huyo aliyejulikana kwa jina la Gracious Sinkala kisha kumtandika fimbo kichwani jambo ambalo lilimsababishia kifo.
“Ukweli wa mambo ni kwamba katika siku hiyo saa kumi na mbili asubuhi, marehemu alijeruhiwa vibaya upande wa kushoto wa kichwa na kusababisha kutokwa na damu nyingi baada ya kudaiwa kupigwa fimbo na mkewe,” imeeleza tovuti hiyo.
Alipelekwa katika zahanati ya Waitwika vijijini lakini baadaye akapewa rufaa katika hospitali ya wilaya ya Nakonde ambapo alifariki dunia.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya wilaya ya Nakonde.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Muchinga, Paul Achiume amethibitishia kutokea kwa tukio hilo na amesema kuwa mshukiwa yuko mikononi mwa polisi hivi sasa akisubiri kufikishwa mahakamani.