Mugabe aeleza alivyomnasa Grace

Muktasari:
- Uhusiano baina yao ulianza wakati mke wa Mugabe aitwaye Sally akipigania uhai wake kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya figo
Harare, Zimbabwe. Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe wiki iliyopita alifichua siri alivyomkumbatia na kumbusu aliyekuwa katibu muhtasi wake, Grace Marufu na huo kuwa mwanzo wa mahusiano yao ya kimapenzi kipindi ambacho mkewe alikuwa akipigania uhai kutokana na ugonjwa wa figo.
Mugabe mwenye umri wa miaka 95 sasa na kiongozi wa muda mrefu, alisema hayo kwenye makazi yake maarufu kama Blue Roof, wakati wa mazishi ya mama mkwe wake, yaani mama yake Grace.
Grace alibaki ametumbua macho wakati mkongwe huyo akieleza kwamba alimpiga tu busu na yeye akaamua kumpenda mzee huyo kwa kuwa hakuonekana kukataa.
Mkongwe huyo na kiongozi wa zamani wa chama cha Zanu PF, muumini kindakindaki wa kikatoliki, alisema aliwekwa katika mazingira magumu ya kuamua ama kutii mafundisho ya Kanisa yanayokataa uzinifu au kumridhisha mama yake ambaye alikuwa anahitaji wajukuu.
Sally hakuwa na watoto kwa sababu ya matatizo ya afya yake.
"Ndiyo, tulianza mapenzi wakati Sally akiwa bado mzima. Ilinilazimu," Mugabe aliwaambia waombolezaji Alhamisi iliyopita wakati wa misa iliyoandaliwa kwa ajili ya mama mkwe wake.
"Grace na mimi hatukuwahi kukutana na kupanga miadi, nilitambulishwa kwake na mimi nikajisemea ni msichana mzuri. Kwa hiyo aliingia kama katibu muhtasi na walikuwapo wengi, niliwatazama tu na baada ya hapo nilimpenda kwa kumwona kwa mara ya kwanza Grace. Kisha nilimwambia siku moja, nakupenda na wala hakunijibu kisha nikamshika mkono kwa nguvu na nikambusu. Hakupinga wala kukataa na kisha nikajisemea moyoni kwamba ikiwa ameridhia kupigwa busu ina maana ananipenda.”