Muswada wa fedha kuigawa Kenya

Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.

What you need to know:

  • Baada ya onyo la Rais William Ruto wa Kenya dhidi ya wabunge watakaothubutu kuupinga Muswada wa Fedha, Naibu wake Rigathi Gachagua ameibuka na kusema wale wote watakaopinga hawatapata maendeleo kwenye maeneo yao.

Kenya. Baada ya onyo la Rais William Ruto wa Kenya dhidi ya wabunge watakaothubutu kuupinga Muswada wa Fedha, Naibu wake Rigathi Gachagua ameibuka na kusema wale wote watakaopinga hawatapata maendeleo kwenye maeneo yao.

 Gachagua ametoa kauli hiyo zikiwa zimepita siku mbili tangu Ruto aseme juu ya muswada huo ambao Serikali ya Kenya Kwanza inautegemea kupata mapato ya kufadhili ajenda yake ya maendeleo katika nchi nzima.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kenya, Gachagua amesema wabunge ambao watapinga muswada huo wasitarajie kupata fedha kwa ajili ya miradi kama vile ujenzi wa barabara.

"Kuna uchochezi mkubwa kuhusu suala nzima la muswada. Jana nilikuwa Kitui na mbunge wao aliongelea kusitisha shughuli na watu wakapiga makofi. Baadaye aliniambia wanahitaji barabara, anatarajia fedha za kujenga barabara zitoke wapi?" alihoji Gachagua alipokuwa katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Leshuta katika kaunti ya Narok juzi Jumapili.

Rais Ruto anataka wabunge kuupigia kura ya wazi Muswada wa Fedha 2023 utakapowasilishwa bungeni wiki hii, huku akitishia kuwakabili watakaoupinga.

Akihutubia juzi jijini Nairobi, Ruto alisema kura ya wazi itamsaidia kuwabaini wabunge wanaopinga ajenda yake ya maendeleo.

“Nataka Wakenya wawajue viongozi ambao wanapinga juhudi zangu kuondoa ukosefu wa ajira. Wale watakaopinga muswada huo ni maadui wa maendeleo,” alionya Ruto.

“Mimi nangoja kuona mbunge ambaye atapinga mpango tulio nao na atasimama upande gani wa hawa wananchi. Nawapa rai wabunge kuupitisha muswada pamoja na hazina ya ujenzi kwani ni mpango mzuri kwa Wakenya,” aliongeza.

Ruto alisema mpango huo utaibua ajira kwa mamilioni ya vijana nchini na utekelezaji wa mpango wa nyumba za bei nafuu ambayo ndiyo njia ya pekee ya kukabili ukosefu wa ajira Kenya.

Akizungumzia ukosefu wa ajira, alisema jumla ya vijana milioni 5 hawana ajira, huku idadi hiyo ikiongezeka kwa vijana 800,000 kila mwaka.

Alisema endapo mswada huo utatekelezwa, Wakenya watatozwa asilimia tatu ya mishahara yao na fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa mpango huo.

Kauli za Ruto na naibu wake Gachagua zinalenga mkakati wa wabunge wa Azimio la Umoja-One Kenya ambao wametishia kuvuruga usomaji wa bajeti iwapo huo utapitishwa bungeni bila marekebisho. Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Opiyo Wandayi amesema wabunge wa upinzani watazua vurugu kuhakikisha Waziri wa Fedha Profesa Njuguna Ndung’u hasomi bajeti iwapo masuala ambayo wameyaibua hayatashughulikiwa.

Wandayi ambaye pia ni mbunge wa Ugunja, amenukuliwa akisema wabunge wote wa ODM wameamrishwa wapinge muswada huo na iwapo utapitishwa watahakikisha wametumia njia nyingine kuhakikisha bajeti yenyewe haisomwi.

“Wakenya wengi wamekataa muswada huu. Sioni kwa nini Bunge linastahili kuupitisha,” alisema Wandayi.

Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga na viongozi wengine wamekuwa wakipinga muswada huo na hata kutishia kuongoza maandamano iwapo utapitishwa.

Baadhi ya wabunge ambao waliandamana na Wandayi kuzungumzia muswada huo ni TJ Kajwang’ (Ruaraka), Adipo Okuome (Karachuonyo), Lillian Gogo (Rangwe) na Rosa Buyu wa Kisumu Mjini Magharibi.

Wandayi na wenzake pia wamewalaumu wabunge wa ODM ambao wamehamia mrengo wa Serikali na sasa wanafanya kazi na Rais Ruto.

Wabunge hao ni Gideon Ochanda (Bondo), Caroli Omondi (Suba Kusini), Elisha Odhiambo (Gem), Mark Nyamita (Uriri), Felix Odiwuor (Lang’ata), Paul Abuor (Rongo) na Walter Owino (Awendo).


Imeandaliwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa  mashirika.