Mwizi wa simu anaswa baada ya kulala fofofo kanisani
Muktasari:
- “Nilifika kanisani saa kumi jioni na kuketi nyuma, nikingoja muda usogee niibe simu za watu ambao wangetaka kuchaji nyuma ya kanisa. Niliiba simu 10 lakini bahati mbaya nililala sikuamka hadi saa 3 asubuhi,” amekiri mwizi Anini.
Nigeria. ‘Hivi ni vituko uswahilini’ unaweza ukasema hivyo, hii ni baada ya Maofisa wa Polisi katika jimbo la Osun nchini Nigeria kumkamata mwizi maarufu wa simu ajulikanaye kwa jina la Saheed Abioye maarufu kama ‘Anini’, baada ya kuiba simu za waumini na kulala fofofo kanisani.
Mtuhumiwa huyo ambaye alinaswa na askari wa Kikosi cha Kupambana na Utamaduni cha Kamandi ya Polisi Jimbo la Osun, amesema siku ya kukamatwa kwake alienda katika kanisa la Osun lililopo mtaa wa Alekuwudo kwa lengo la kuwaibia simu waumini wakati wa ibada ya mkesha lakini badala yake alijikuta analala baada ya maombi kuanza kanisani hapo.
“Nilifika kanisani saa kumi jioni na kuketi nyuma, nikingoja muda usogee niibe simu za watu ambao wangetaka kuchaji nyuma ya kanisa. Niliiba simu 10 lakini bahati mbaya nililala sikuamka hadi saa 3 asubuhi.
“Nilipozinduka, mkesha ulikuwa umeisha na watu walikuwa tayari wanarudi nyumbani, hivyo nikashikwa baada ya kujaribu kuondoka,” amesema Anini wakati akihojiwa na Polisi.
Anini pia amekiri kwa Polisi kuwa ameshaiba na kuuza simu zaidi ya 18 kutoka maeneo mbalimbali katika jimbo hilo.
Kwa mujibu wa tovuti ya GHPage imesema kwa amri ya Polisi Anini atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.