Mzimu wa mapinduzi ya kijeshi unavyoitafuna Afrika
Muktasari:
- Mapinduzi ya Gabon yametokea wakati kukiwa na mapinduzi mengine katika nchi za Niger, Burkina Faso, Mali, Guinea, Guinea-Bissau.
Dar es Salaam. Mapinduzi ya Rais wa Gabon, Ali Bongo yameendeleza vuguvugu la mapinduzi katika ukanda wa Afrika Magharibi tangu mwaka 2020.
Mapinduzi hayo yametokea ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitatu tu, yakijumuisha nchi za Niger, Burkina Faso, Mali, Guinea, Guinea-Bissau, na sasa Gabon.
Agosti 30, 2023 viongozi wa jeshi la nchi hiyo walitangaza kumweka kizuizini Rais Bongo muda mfupi baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza kiongozi huyo aliyekuwa akigombea muhula wa tatu, kuwa ni mshindi.
Maofisa hao wa jeshi walijitokeza kwenye televisheni ya Taifa na kusema wamechukua mamlaka, kufunga mipaka ya nchi hiyo pamoja na kuvunja taasisi zote za serikali.
Jumamosi ya juma lililoisha wananchi walipiga kura kumchagua Rais, wabunge pamoja na Serikali za mitaa ambapo Ali Bongo alikuwa akigombea Urais huku akichuana na mpinzani wake Albert Ossa.
Upinzani ulidai kuwa matokeo hayo yalikuwa ya udanganyifu baada ya kutangazwa kuwa Bongo amepata asilimia 64 ya kura zilizopigwa.
Kushinda kwa Bongo kungemfanya aendelee na muhula wa tatu kuiongoza nchi hiyo ya Afrika ya Kati kwa kipindi kingine cha miaka saba kama katiba ya nchi inavyosema.
Kupinduliwa kwa Bongo kunatamatisha uongozi wa familia yake iliyodumu kwa miaka zaid ya 50 madarakani nchini humo ambapo baba yake pekee Omar Bongo Ondimba aliiongoza nchi hiyo kwa miaka 42 kabla ya mwanaye kutwaa madaraka.
Ali Bongo alichukua madaraka mwaka 2009 baada ya kifo cha baba yake na kutawala kwa miaka 14 hadi uchaguzi uliofanyika Agosti 26 mwaka huu ambao ungemuweka madarakani hadi 2030.
Maandamano mengine
Kauli nyingi za majeshi hayo zinalalamikia kuhusu Serikali husika kushindwa kutekeleza majukumu yake, ung’ang’anizi wa madaraka pamoja na kuzorota hali ya usalama.
Mapema mwaka huu aliyekuwa Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita alipinduliwa na maofisa wa jeshi la nchi hiyo kwa kulazimishwa kujiuzulu na baadaye ikaundwa serikali ya mpito.
Kanali Assimi Goïta, ambaye aliongoza mapinduzi hayo mwaka mmoja baadaye alitangaza kuwa ametwaa mamlaka kutoka kwa Rais wa mpito Bah Ndaw, na Waziri mkuu Moctar Ouane, waliohudumu kwa miezi kadhaa ikidaiwa walishindwa kushauriana naye kuhusu kuundwa kwa serikali mpya.
Baadaye mzimu ukaamia nchini Guinea mnamo Septemba 2021, Kanali Mamady Doumbouya alimpindua Rais Alpha Condé mwaka mmoja baada ya kushinda muhula watatu.
Conde, mwenye umri wa miaka 83, alizuiliwa na wanajeshi wa kikosi maalum (GFS) mnamo Septemba, 5 muda mchache baada ya kuripotiwa kwa ufyatulianaji wa risasi karibu na makazi ya rais huko Conakry.
Kapteni Ibrahim Traore ambaye aligonga vichwa vya habari hivi karibuni kwenye mkutano wa viongozi wa afrika na Urusi, yeye aliongoza mapinduzi mnamo Septemba, 2022 nchini Burkina Faso yaliyomtoa Rais wa mpito Paul Sandaogo Damiba aliyetanguliwa na Rais Roch Kabore aliyepinduliwan 2022
Nchini Niger nako mapinduzi yalifanywa na wanajeshi wakiongozwa na, Jenerali Abdourahamane Tchiani ambao waliopewa jukumu la kumlinda Rais Mohamed Bazoum.
Nchini Guine Bissau lilifanyika jaribio la mapinduzi kumpindua Rais Umaro Sissoco Embalo mwaka 2022, lililotokea jijini Bissau na kusababisha vifo vya watu 11.
Watu waliojihami kwa silaha, wamivamia majengo ya serikali jijini Bissau wakati Rais Umaro Sissoco Embalo, alipokuwa katika kikao na Mawaziri wake na kuanza kufyatua risasi.
Rais Embalo, alisema aliponea kuuawa wakati wa makabiliano ya risasi yaliyodumu kwa saa tano kwa lengo la kuindoa serikali yake.
Wachambuzi
Mtaalamu na mchambuzi wa siasa za maridhiano Afrika, Ezekiel Kamwaga alisema changamoto ni mfumo wa kidemokrasia ambapo watawala na watawaliwa imeonekana kutokuwa na muunganiko kwa kushindwa kutatua kero za wananchi.
“Tumeona nchi hizo wa wale wanaopindua wameonekana kushangiliwa na wananchi sasa inaonyesha namna gani hakuna muunganiko kati ya wananchi na viongozi,” alisema Kamwaga.
Alisema kuna changamoto ya kuwa na viongozi wanaojidai wanaendesha nchi zao kidemokrasia kumbe ukweli hakuna akitolea mfano familia ya Bongo.
Naye, Mchambuzi wa masuala ya siasa Said Msonga, ameitwisha mzigo umoja wa Afrika (AU), kutimiza wajibu kuhakikisha mataifa ya Afrika yanajikomboa kwenye ukoloni.
Msonga amesema bado kuna mataifa yamejiegemeza kwenye makoloni yao ya zamani ambao wananufaika na rasilimali za nchi hizo ambazo ndio chanzo cha wanajeshi kutwa madaraka.
“Jambo hilo la mapinduzi halikubaliki lakini hadi yanatokea basi kuna tatizo na tatizo hilo linapaswa litatuliwe, ndio maana AU inapaswa isimamie kuhaklikisha kwamba mataifa yanajijenga kuwa na mfumo bora wa uongozi,” amesema Msonga.