Prime
Padri mwingine auawa kwa kumininiwa risasi akielekea ibadani

Muktasari:
- Padri Allois Bett wa Parokia ya St Matthias Mulumba Tot ameuawa jana eneo la Makoro katika Kijiji cha Kabartile baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Moshi/Nairobi. Siku chache baada ya kutekwa na kuuawa kwa Paroko wa Parokia ya Igwamiti ya Kanisa Katoliki huko Nyahururi nchini Kenya, Padri John Maina, Padri mwingine, Allois Bett inadaiwa ameuawa kwa kumiminiwa risasi nchini humo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Peter Mulinge, Padri Bett ameeleza kabla ya kifo chake kuwa alimiminiwa risasi na watu waliokuwa na silaha akiwa njiani wakati anaelekea ibadani kanisani katika eneo la Tot, Bonde la Kerio.
Tukio la kuuawa kwa Padri Bett wa Parokia ya St Matthias Mulumba Tot limetokea jana Alhamisi Mei 22, 2025 eneo la Makoro katika Kijiji cha Kabartile baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha za moto.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Msemaji wa Huduma ya Polisi (NPS) nchini Kenya, Muchiri Nyaga, imesema baada ya kupokewa kwa taarifa hiyo, polisi walianzisha msako na tayari watu sita wanashikiliwa.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha tukio hili halina uhusiano na wizi wa mifugo au ujambazi. NPS inalaani kitendo hiki kiovu na imejitolea kufanya zuio za kina na za haraka ili kuwatia nguvuni wale wote waliohusika katika uhalifu huo,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa “Tunaiomba jamii katika eneo kulipotokea mauaji kuwa watuliu na kuendelea shughuli zao na kutoa ushirikiano kwa NPS. Tunaomba yeyote mwenye taarifa sahihi za tukio hili atupatie.”
Mbunge wa Marakwet Magharibi, Timoth Toroitich ameomboleza kifo hicho kwa kueleza kuwa, “Padri Bett alikuwa mtu wa imani thabiti. Alikuwa akinipigia simu mara kwa mara kunitia moyo na kunihimiza hasa nyakati ngumu.”
Katika mitandao ya kijamii, wamemuelezea padri kama kiongozi wa kiroho aliyefanya majukumu ya kijamii pia kama kutoa ushauri katika maendeleo zikiwamo shule ya wavulana Chebiemit na wasichana Kapkoros.
Mbunge huyo amesema damu iliyomwagika ya Padri Bett itanyunyizia mti wa amani katika bonde la Kerio, huku akiapa kuwa urithi wa padri huyo utaendelea kuwa chanzo cha uponyaji na umoja katika eneo hilo.
Paroko aliyouawa
Tukio la kuuawa kwa Padri Bett, limekuja siku chache tangu kuuawa kwa Padri Maina ambaye kifo chake kulihusishwa na masuala ya kisiasa.
Kulingana na taarifa ya Polisi, Ilibainika Padri Maina alikuwa akifuatiliwa na baadhi ya watu waliokuwa wakimtaka awagawie pesa alizodaiwa kupewa baada ya kufanyika jubilee ya miaka 25 parokiani kwake.
Taarifa ya Polisi iliyotolewa Mei 20, 2025 na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) nchini Kenya, kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), imewataka raia wa Kenya kuwa watulivu kutokana na uvumi mitandaoni.
DCI amebainisha padri huyo alipatikana Mei 15, 2025 kando ya barabara ya Nakuru akiwa na majeraha kichwani na alimweleza msamaria aliyemwokota kuwa alikuwa ametekwa katika Parokia yake, iliyopo umbali wa kilometa 40.
Ingawa taarifa hiyo ya DCI iliyowekwa katika akaunti rasmi ya DCI haikueleza ilipo gari yake aina ya Subaru Forester, lakini taarifa katika mitandao ya kijamii zilieleza kuwa gari lake hilo halijapatikana na halijulikani liko wapi.
Taarifa hiyo ya DCI inasema Aprili 27, 2025, Padri Maina alihudhuria Jubilei hiyo na ibada ya kuwekwa wakfu kwa Padri Simon Thuita.
“Licha ya jitihada za wahudumu wa afya, Padri Maina alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu,” ameeleza DCI.
“Mwili wake ulihamishiwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Kaunti Ndogo ya Nyahururu kutokana na ombi la waumini wenzake kwa ajili ya kuhifadhiwa na kufanyiwa upasuaji wa uchunguzi wa sababu zilizosababisha kifo chake,” ameeleza.
Kwa mujibu wa DCI, Mei 19, 2025, upasuaji wa maiti ulifanywa na daktari wa serikali na matokeo ya awali yalionesha kuwa majeraha ya kichwani aliyokuwa nayo Padri Maina huenda hayakuwa chanzo cha kifo chake.
Mwanapalotholia wa Serikali, Titus Ngulungu ndiye aliyefanya uchunguzi wa mwili wa Padri huyo katika Hospitali ya Papa Benedict Catholic, lakini taarifa nyingine ambazo hazijathibitishwa zilidai alipigwa na kitu butu kichwani.
Naibu Mkuu wa Dayosisi ya Nyahururu, Padri Timothy Maina pamoja na mapadri wengine 10 na ndugu wa marehemu walihudhuria uchunguzi huo, huku taarifa zingine zikidai mwili ulikuwa umejaa damu na majeraha yanayoonekana ni risasi.
“Hivyo, sampuli zilichukuliwa na kupelekwa kwa uchunguzi zaidi wa kimaabara,” ameeleza DCI katika taarifa hiyo inayopigwa mitandaoni.
DCI katika taarifa hiyo ameeleza kuwa maofisa wa upelelezi kutoka katika ofisi hiyo wanachunguza taarifa kwamba Padri Maina alikuwa ameeleza kuwa maisha yake yalikuwa hatarini, ingawa hakuwahi kuripoti hilo katika kituo chochote cha polisi.
Maofisa wa upelelezi wanaendelea kufuatilia ushahidi wa kitaalamu ili kuunda upya matukio ya mwisho ya Padri Maina na kuwakamata watuhumiwa huku ikiwaomba wananchi wenye taarifa sahihi kuziwasilishwa kwao.
“DCI amewahimiza wananchi kubaki watulivu kutokana na uvumi wa mitandaoni. Timu yetu ya wachunguzi inafanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu ili kulitatua suala hili kwa umakini ili kuhakikisha haki inapatikana,” amesema.
Habari hii imeandikwa kwa msaada wa mitandao mbalimbali ya Kijami