Polisi aliyemuua George Floyd ahofiwa kuchomwa kisu gerezani

Muktasari:

  • Ofisa wa Polisi kutoka nchini Marekani aliyekutwa na hatia ya kutekeleza mauaji ya George Floyd anadaiwa kuchomwa kisu akiwa gerezani. Ikumbukwe mauaji ya mmarekani huyo yalitikisa dunia mwaka 2020 ambapo maelfu waliandamana hadi kuanzisha harakati za haki ya mtu mweusi, ‘Black Lives Matter’.

Dar es Salaam. Aliyekuwa ofisa wa Polisi wa Minneapolis nchini Marekani, Derek Chauvin ambaye alikutwa na hatia ya kutekeleza mauaji ya Mmarekani George Floyd amedaiwa kuchomwa kisu akiwa gerezani.

Chauvin, (47) amedaiwa kushambuliwa na mfungwa mwenzie wakiwa gerezani Arizona Ijumaa mwishoni mwa juma hili, Tovuti ya Sky News imeandika.

Ofisi ya Magereza ya Marekani imethibitisha kuwa kuna mfungwa ameshambuliwa kwenye Taasisi ya Shirikisho ya Urekebishaji (FCI) huko Tucson majira ya saa 12:30 jioni kwa saa za Marekani.

Japokuwa halikutajwa jina la muathiriwa inaelezwa kuwa wafanyakazi wa magereza walichukua hatua za kuokoa maisha ya Chauvin, kabla ya kukimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi.

Katika taarifa nyingine Shirika la FBI pia limesema linafahamu kuhusu shambulio katika gereza hilo ingawa halikutaja mtu yeyote aliyehusika.

Chauvin alihukumiwa kifungo cha miaka miaka 21 kwa kukiuka haki za kiraia za Floyd pia miaka mingine 22 jela kwa mauaji ya shahada ya pili mnamo Mei 2020 kwa kumkandamiza shingoni na goti lake kwa zaidi ya dakika tisa wakiwa barabarani.

Mauaji hayo, ambayo yalirekodiwa kwenye simu na mpita njia, yalimuonesha Floyd akisema ‘Siwezi kupumua’, yalizua maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi kote ulimwenguni.