Aliyemuua Floyd atupwa jela miaka 21, atoa neno

Muktasari:

Mahakama ya Mji wa Minneapolis, Minnesota nchini Marekani imemuhukumu kifungo cha miaka 21 na nusu jela ofisa wa polisi, Derek Chauvin baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Mmarekani mweusi, George Floyd Mei mwaka juzi na kusababisha maandamano yaliyotikisa dunia.

Minnesota. Mahakama ya Mji wa Minneapolis, Minnesota nchini Marekani imemuhukumu kifungo cha miaka 21 na nusu jela ofisa wa polisi, Derek Chauvin baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Mmarekani mweusi, George Floyd Mei mwaka juzi na kusababisha maandamano yaliyotikisa dunia.

Chauvin anakwenda jela baada ya Mahakama ya Minnesota kujiridhisha pasipo shaka alitenda makosa ya kutumia vibaya nafasi aliyoaminiwa na mamlaka yake kisha kufanya ukatili dhidi ya Floyd, kutenda kosa hadharani huku watoto wakishuhudia na kutenda kosa kwa kushirikiana na watu wengine (watatu) kinyume na sheria za Minnesota.

“Ninatoa salamu zangu za pole kwa familia ya Floyd,” haya yalikuwa maneno ya mwisho ya Chauvin kabla hukumu yake kusomwa.

Kwa mujibu wa sheria za Minnesota, Chauvin atatakiwa kutumikia robo tatu au miaka 15 ya kifungo jela.


Kwa nini ni hukumu ya kihistoria

Kwa mujibu wa mwongozo wa utoaji adhabu mjini Minnesota, mtu anapaswa kufungwa jela kwa muda usiozidi miaka 10 hadi 15, ambacho ni kiwango cha juu cha adhabu dhidi ya makosa ya jinai, lakini kwa Chauvin mwongozo huo umewekwa kando na atatumikia adhabu kwa miaka 21 na miezi sita.

Jaji aliyesikiliza kesi hiyo, Peter Cahill alisema adhabu hiyo haijafuata mihemko wala mawazo ya watu.

“Nimezingatia zaidi maumivu ambayo familia ya Floyd imeyapata na inayo hadi leo,” ameandika Jaji Cahill katika hukumu hiyo iliyochapishwa kwenye kurasa 22, ikitajwa kuwa hukumu kali mno kwa Chauvin.

Makosa mengine ya Chauvin ni kutumia vibaya nafasi yake pamoja na mamlaka aliyopewa.

Katika hukumu hiyo, Jaji Cahill alisema Chauvin bila heshima alimdhulumu Floyd “utu” wake ambao ni haki ya kila binadamu.

Picha ya video iliyomuonyesha Chauvin akimkandamiza shingo Floyd bila kumpa nafasi hata ya kupumua kwa muda mrefu ni dhahiri alimsababishia maumivu yasiyomithilika.

“Yalikuwa mauaji ya maumivu na mateso ya kiwango cha juu sana,” inasomeka sehemu ya hukumu ya Jaji Cahill.

Kesi hii pia inabaki kuwa ya historia katika mwenendo wa usikilizwaji wake baada ya kumkuta Chauvin na hatia.

Jopo la waendesha mashtaka wa Serikali lilipendekeza apewe adhabu ya miaka 30 jela hatua ambao jopo hilo lilisema inaweza kuifuta zaidi mochozi familia ya Floyd na jamii ya watu weusi.

Hata hivyo, Chauvin aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kutazama historia yake kuwa hana historia yeyote ya kutenda makosa nchini humo.


Ilivyokuwa

Chauvin alitenda kosa hilo akiwa na wenzake watatu eneo la tukio, Tou Thao, Thomas Lane na Alex Kueng.

Akiwa na wenzake Chauvin alimuua Floyd kwa kumbana shingo kwa nguvu akitumia goti kwa muda wa dakika 9 na sekunde 29 bila kumpa pumzi na alisikia kilalama kwa mbali kuwa hawezi kupumua alipokamatwa na askari huyo kwa madai ya kufanya malipo katika duka moja kwa kutumia noti bandia.

Vitendo vya polisi kuua raia Marekani vilikuwa vikiongezeka mara kwa mara, ndani ya miezi mitano ya mwaka 2021, watu 371 walifyatuliwa risasi na polisi kati yao 71 wakiwa watu weusi.

Mwaka 2020 hali ilitajwa kuwa mbaya zaidi ambapo watu 1,021 walipigwa risasi na polisi.

Katika matukio hayo ndani ya miaka miwili, idadi ya Wamarekani weusi inaongoza kwa kushambuliwa kwa risasi na polisi ikiringanisha na makundi mengine yanayopatikana nchini humo.