Polisi aliyetekwa, ashtakiwa kwa uzembe kupoteza silaha
Ofisa wa Polisi Fredrick Kinaibei.
Dar es Salaam. Ofisa wa Polisi Fredrick Kinaibei katika Kaunti ya Narok nchini Kenya amejikuta akimalizia wikiendi yake akiwa sero baada ya kushtakiwa kwa uzembe wa kupoteza silaha.
Ofisa huyo ameshtakiwa baada ya uchunguzi uliofanywa na maofisa wenzake na kubaini kwamba amepoteza silaha yake kwa uzembe.
Kinabei anashtakiwa kwa makossa mawili ikiwamo uzembe uliosababisha upotevu wa silaha ikiwa na risasi 14 na shtaka la pili ni kutoa maelezo ya uongo kwa mtumishi aliyeajiriwa na umma.
Awali, Jumatano Februari 8, 2023 Kinabei alikutwa akiwa ametupwa karibu na mto baada ya kutekwa na watu wasiojulikana katika Kaunti ya Narok.
Katika maelezo yake yaliyowasilishwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi kutokana na tukio hilo, alieleza alitekwa na kundi la watu wakati akikaribia kuingia kwenye geti la nyumbani kwake.
“Niliingizwa kwenye gari aina ya Toyota Wish ambayo namba zake hazijulikani na walinipeleka kuelekea Mau, Kaunti ya Narok,” inaeleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, mke wake alitoa taarifa polisi kuhusu kutoonekana mume wake huyo ambaye ni ofisa wa polisi.
Maofisa wenzake walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika na utekaji huo.