SADC yahimiza vikosi vya waasi kumaliza mzozo DRC

Rais Samia Suluhu Hassan (wa kwanza kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kabla ya kuanza kwa Mkutano wa dharura wa nchi hizo Organ Troika, SADC Troika leo Jumatatu Mei 8, 2023 nchini Namibia.
Muktasari:
- Vikundi vyenye silaha kali vinavyotekeleza mashambulizi Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) vimeagizwa kutupa silaha zao wakati Jeshi la SADC kutoka kikosi cha kudumu cha jumuiya hiyo kikiidhinishwa ili kuiunga mkono nchi hiyo kuweza kurejesha amani na usalama.
Dar es Salaam. Mkutano wa kujadili hali ya Usalama wa Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umetoa wito kwa vikundi vyenye silaha kusitisha uhasama na kujiondoa bila masharti katika maeneo wanayoyashikilia nchini humo.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano huo huku washiriki wengine wakiwa ni Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Troika na Nchi zinazochangia Vikosi vya Jeshi vya Force Intervention Brigade (FIB).
Mkutano huo uliofanyika leo Mei 8, 2023 jijini Windhoek nchini Namibia pia umewasihi wanachama wa SADC kuunga mkono Serikali ya DRC na kushughulikia hali ya usalama ya Mashariki mwa nchi hiyo kabla ya uchaguzi.
Kufanyika kwa mkutano huo kunatokana na mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na watu wenye silaha kali nchini DRC ambao kwa vipindi tofauti wamekuwa wakisababisha maafa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus imeeleza kuwa mkutano huu unatarajiwa kufanyika tena Desemba 2023.
"Vilevile mkutano huo umesisitiza uungwaji mkono wa DRC katika mapambano dhidi ya makundi ya kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo ili kuleta amani endelevu, usalama na ustawi kwa wananchi wa Congo na Jumuiya ya SADC kwa ujumla," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa hatua nyingine, mkutano huo umeidhinisha kupeleka Kikosi cha Jeshi la SADC kutoka kikosi cha kudumu cha jumuiya hiyo ili kuiunga mkono DRC iweze kurejesha amani na usalama.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano huo ni Rais wa Namibia Dk Hage Geingo, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais wa DRC Félix Tshisekedi, Waziri wa Mahusiano ya Mambo ya Nje wa Angola, Balozi Tete Antonio, Waziri wa Ulinzi wa Malawi, Harry Mkandawir pamoja na Balozi wa Zambia chini Namibia Stephen Katuka.