Waasi wa M23 wauteka mji wa Kitshanga, mashariki mwa DRC

Muktasari:

  • Kikosi cha waasi cha M23 wamefanikiwa kuteka mji wa Kitshanga, mashariki mwa DRC, ambapo wamesema wanawashutumu wanajeshi wa serikali kwa kushambulia raia huko Kitchanga na kwingineko, na kusema kundi la waasi linalazimika kuingilia kati na kukomesha mauaji mengine ya kimbari.

Dar es Salaam. Waasi wa M23 wameuteka mji wa kimkakati wa Kitshanga uliopo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) baada ya siku kadhaa za mapigano makali.

Kwa mujibu wa kituo cha habari Al Jazeera, jeshi la DRC Ijumaa iliyopita lilithibitisha vikosi vyake kuondoka, likitaja kuwa ni mbinu ya kuwalinda raia katika kukabiliana na mashambulizi mapya ya wapiganaji hao.

“Tumejiondoa kwa busara ili kuepuka hali mbaya zaidi kwa watu wetu huko Kitshanga,” alisema Luteni Kanali Guillaume Ndjike, msemaji wa Gavana wa kijeshi wa Kivu Kaskazini.

Inaelezwa waasi walichukua udhibiti wa Kitshanga Alhamisi Januari 26, 2023 baada ya kuteka vijiji kadhaa kwenye barabara inayounganisha mji wa takribani watu 60,000 na mji mkuu wa mkoa wa Goma ulio umbali wa kilomita 90.

Video kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha wapiganaji wa kundi la M23 wakisherehekea na kudai kuwa wameuteka mji huo.

Msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka katika taarifa yake ya Alhamisi iliyopita alishutumu wanajeshi wa serikali kwa kushambulia raia huko Kitchanga na kwingineko na kusema M23 inalazimika kuingilia kati ili kukomesha mauaji mengine ya kimbari.

Vyanzo vya habari katika jeshi la Congo vilisema kuwa siku mbili zilizopita kikosi cha wanajeshi kilivuka kutoka Rwanda ili kuimarisha M23.

Hilo liliwasaidia waasi kuchukua udhibiti wa Kitshanga. Na hiyo inamaanisha kuwa M23 sasa wanadhibiti barabara kutoka Kitshanga hadi Goma.”

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC (Monusco) umesema zaidi ya watu 500, wakiwemo wanawake na watoto, wanatafuta hifadhi.

Msemaji wa Monusco, Ndeye Khady Lo alisema raia wanaokimbia kutoka Kitchanga wamepewa mahema, chakula, maji na huduma ya kwanza.

“M23 lazima wakomeshe uhasama wote na waondoke kwenye maeneo waliyoyavamia,” amesema.