Somalia yamtimua balozi wa Ethiopia kutokana na sakata la bandari

Balozi wa Ethiopia nchini Somalia, Mukhtar Ware

Muktasari:

Ethiopia ambayo haina bandari ilikubali mkataba wa maelewano Januari 2024 ili kukodisha kilomita 20 za ukanda wa pwani huko Somaliland eneo ambalo Somalia inasema inalimiliki

Somalia. Serikali ya Somalia imemtimua balozi wa nchi ya Ethiopia, Mukhtar Ware, leo Alhamisi ya Aprili 4, 2024 kutokana na kuongezeka kwa mvutano kuhusu mpango wa bandari huku kukiwa na madai ya kuingilia mambo ya ndani,  Tovuti za Reuters, TRT, na The East African zimeripoti.

Inaelezwa kuwa, Ethiopia ambayo haina bandari ilikubali mkataba wa maelewano Januari 2024 ili kukodisha kilomita 20 za ukanda wa pwani huko Somaliland eneo ambalo Somalia inasema inalimiliki.

Pia, Ethiopia ilisema inataka kuanzisha kituo cha jeshi la wanamaji katika eneo hilo na kuweka uwezekano wa kuitambua Somaliland inayodaiwa kujitenga hali iliyosababisha kuibua hofu kuwa mpango huo unaweza kuiyumbisha pembe ya Afrika.

Ethiopia na Hargeisa, mji mkuu wa Somaliland walitia saini mkataba wa maelewano (MoU) kuhusu ushirikiano ambao ndio uliruhusu Ethiopia kukodisha bandari hiyo iliyoko huko Somaliland.

Katika kupinga kutiwa saini kwa makubaliano hayo, Somalia ilimwita balozi wake mjini Addis Ababa.

Vilevile kilichozidisha mvutano huo zaidi ni baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia kupokea ujumbe kutoka eneo la Puntland linalodaiwa kuwa huru hapo jana Jumatano.

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud aliutaja mpango huo kuwa kinyume cha sheria na mapema Februari akisema nchi yake itajilinda ikiwa Ethiopia itaendeleza makubaliano yake na Somaliland.

Hata hivyo, kuhusu sakata la kutimuliwa kwa balozi huyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, Nebiyu Tedla amesema hana taarifa kuhusu suala hilo.